Ijumaa, tarehe 24 Oktoba, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe Pili Jamadil Awwal 1447 Hijria sawa na tarehe 24 Oktoba 2025.
Siku kama ya leo miaka 1056 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia malenga wa Kiirani, Abu Is'haq Kesa-i Marvazi.
Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasamani na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa kuhusu tawala hizo mbili.
Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (SAW) na kizazi chake, hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as).
Kesa-i Marvazi mbali na kusifika kwa utunzi wa mashairi, lakini pia alitoa waadhi na hikma kupitia mashairi yake ya Kifarsi. Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha diwani ya mashairi.

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita sawa na tarehe Pili mwezi Aban mwaka 1307 Hijria Shamsia, Ayatullah Dakta Sayyid Muhammad Husseini Beheshti mwanafikra na mwanamapinduzi wa Iran, alizaliwa huko Isfahan, moja kati ya miji ya katikati mwa Iran.
Ayatullah Beheshti alilelewa katika familia ya kidini na alianza kujifunza masomo ya kidini akiwa kijana mdogo. Akiwa na umri wa miaka 18, alielekea katika mji wa kidini wa Qum nchini Iran na kusoma kwa maulamaa wakubwa wa mji huo akiwemo Imam Khomeini (RA). Wakati huo huo, Dakta Beheshti alitumia kipawa chake kikubwa na kuamua kuendelea pia na masomo ya Chuo Kikuu na kufanikiwa kupata shahada ya udaktari katika falsafa.
Dakta Beheshti aliuawa shahidi akiwa na viongozi na shakhsiya wengine 72 wa Iran katika mkutano mwezi Tiir mwaka 1360 Hijria Shamsia baada kundi la kigaidi la Munafiqin kuripua bomu katika mkutano huo.
Tarehe 24 Oktoba miaka 96 iliyopita ulianza mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa Marekani unaojulikana kwa jina la Wall Street.
Kimsingi Wall Street ni mtaa mashuhuri mjini New York ambao kutokana na kuwa na taasisi nyingi kubwa za kifedha na kibenki unatambuliwa kuwa kituo muhimu sana cha kiuchumi cha Marekani. Kituo hicho cha kiuchumi kilikumbwa na mgogoro mkubwa wa kifedha wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na baada yake.
Oktoba 24 mwaka 1929 janga kubwa la kifedha liligubika makao ya hisa ya Marekani huko Wall Street na kupelekea kukosa kazi zaidi ya wafanyakazi milioni 13 wa Marekani, njaa kali, kufilisika kwa viwanda na mabenki na mamilioni ya watu kupoteza makazi na nyumba zao.

Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, Umoja wa Mataifa ulichukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa.
Wawakilishi wa mataifa yaliyoafikiana katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, yaani Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa, waliandaa mazingira ya kuundwa umoja huo; na hatimaye katika mkutano uliofanyika San Francisco, Marekani, wawakilishi kutoka nchi 50 duniani walipitisha sheria za kuundwa umoja huo.
Ijapokuwa umoja huo umefanikiwa katika baadhi ya mambo, lakini kuwepo haki ya veto kwa baadhi ya nchi ambazo ni Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, na China kunalifanya Baraza la Usalama la umoja huo kufuata kibubusa siasa za nchi zenye haki ya kupiga kura ya turufu, na hasa Marekani.

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, Iran ilifanikiwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa hati ya Umoja wa Mataifa, mlango wa kujiunga na umoja huo uko wazi kwa mataifa yote yanayopenda amani na ambayo yanakubaliana na sheria na maaamuzi ya taasisi hiyo.
Nchini Iran, Umoja wa Mataifa una jumla ya ofisi 14 za uwakilishi na utendaji.

Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, vita vya nne baina ya Waarabu na Israel vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Ramadhani vilifikia tamati.
Tarehe 6 Oktoba 1973 Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri akiwa na lengo la kufidia kushindwa katika vita vya Waarabu na Israel mwaka 1967, alifanya mashambulio ya kushtukiza katika ngome za Israel katika Mfereji wa Suez.
Muda mchache baada ya mashambulio hayo, wanajeshi wa Syria nao walifanya mashambulio katika miinuko ya Golan ambayo ilikaliwa kwa mabavu na Israel katika vita vya mwaka 1967 na kufanikiwa kuwatimua wanajeshi wote wa utawala huo haramu kutoka katika maeneo waliokuwa wakiyadhibiti.

Na siku kama ya leo miaka 36 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Allamah Mirza Jawad Agha Tehrani.
Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea katika miji mitakatifu ya Qum na Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa.
Allamah Mirza Jawad Agha Tehrani alisifika sana kwa uchamungu, zuhudi na kuwapenda sana Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ni Aine Zendegi na Mizanul Matwalib.