Upeo wa ubaguzi; Trump ataka Ilhan, Tlaib wafukuzwe Marekani
Rais Donald Trump amesema Wawakilishi wa Marekani, Ilhan Omar na Rashida Tlaib wanapaswa kurudishwa "walikotoka" baada ya wabunge hao wawili wa chama cha Democratic katika Congress ya Marekani kupiga kelele na kulalamika wakati wa hotuba ya karibuni ya Trump katika Kongresi.
Trump ameandika kwenye mtandao wake wa Truth Social Jumatano jioni kwamba, wabunge hao wawili Waislamu ni "wanasiasa wapotovu na wala rushwa" ambao wanapaswa kutimuliwa Marekani.
"Unapowatazama Ilhan Omar na Rashida Tlaib wenye akili ndogo, walipopiga kelele bila kudhibitiwa jana (juzi) usiku katika mkutano wa kifahari wa Hali ya Muungano, tukio muhimu na zuri kama hilo, walikuwa na macho yaliyojaa damu za watu wendawazimu, WAPUMBAVU, punguani wa akili na wagonjwa ambao, kusema ukweli, wanaonekana kama wanapaswa kudhibitiwa," Trump ameandika.
"Wakati watu wanaweza kujifanya hivyo, na wakijua kwamba wao ni Wanasiasa Wapotovu na Wafisadi, wabaya sana kwa Nchi yetu, tunapaswa kuwarudisha walikotoka - haraka iwezekanavyo," Trump ameendelea kubwabwaja.
Omar na Tlaib walikuwa miongoni mwa kundi dogo la wabunge wa chama cha Democratic waliopaza sauti kulalamika, wakati wa hotuba ya Trump ya karibu saa mbili siku ya Jumanne.
Huko nyuma, mwakilishi Ilhan, mwanamke wa Kiislamu wa chama cha Democratic alifukuzwa katika Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Baraza la Wawakilishi la Marekani kwa kuukosoa utawala wa Kizayuni wa Israel.