Ni Argentina dhidi ya Uhispania, Waingereza wapigwa mweleka
Lionel Messi na Argentina watacheza na Uhispania katika fainali ya Kombe la Dunia Jumapili ijayo baada ya kuifunga England mabao mawili katika dakika sita na sekunde 24 mwishoni mwa mechi kali ya nusu fainali na kuwavunja mioyo Waingereza.
England iliongoza kuanzia dakika ya 55 kupitia Anthony Gordon na ilionekana tayari kuingia fainali ya kwanza ya Kombe la Dunia tangu 1966, lakini Enzo Fernandez alifunga bao la kusawazisha kutoka nje ya eneo la hatari dakika ya 85 na kisha mchezaji aliyetoka benchi, Lautaro Martinez, akakamilisha kazi kwa Argentuna kwa bao la kichwa dakika ya pili ya nyongeza.
Leo Messi amesaidia kutiwa kimiani mabao yote mawili. Sasa Messi ametoa pasi 12 za mabao katika fainali za Kombe la Dunia, na kuweka rekodi mpya katika uwanja huo.
Timu hizi mbili hazijakuna kwa miaka 21, lakini mazingira ya kabla ya mechi ya jana yalijikita kwenye migogoro mikali ya miaka ya nyuma, ikiwa ni pamoja na migogoro ya Kombe la Dunia na Vita vya Falklands vya 1982, ambavyo vimesikika katika nyimbo za wachezaji na mashabiki wa Argentina.
Kwa ushindi huo, Argentina itamenyana na Hispania katika fainali ya Kombe la Dunia 2026, huku England ikivaana na Ufaransa katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu.
Nukta ya kuashiria ni kwamba wachezaji wa timu ya taifa ya Argentina waliinua bango lililotangaza kwamba "Malvinas ni mali ya Argentina" baada ya kuichapa Uingereza na kufikia fainali ya Kombe la Dunia. Ujumbe huo unahusu Visiwa vya Falkland ambavyo Argentina inadai vilinyakuliwa na mkoloni Mwingireza, na kufufua mzozo wa mamlaka ya visiwa hivyo. Jambo ambalo limeibua mjadala na maswali kuhusu marufuku ya FIFA dhidi ya kuonyeshwa nembo za kisiasa kwenye mashindano hayo.
Je, FIFA itaiadhibu Argentina na wachezaji waliobeba bango lenye ujumbe huo? Wakati utasema…