Uchaguzi wa urais nchini Zambia kufanyika wiki hii
-
Rais Hakainde Hichilema anawania kuchaguliwa kwa muhula mwingine.
Raia wa Zambia waliotimiza masharti ya kupiga kura, Alkhamisi ya wiki hii wataelekea katika vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa rais unaofuatiliwa kwa karibu na ambao utakuwa kipimo cha mafanikio ya kiuchumi ya Rais wa sasa Hakainde Hichilema anayewania kuchaguliwa kwa muhula mwingine.
Hichilema anakabiliwa na upinzani toka kwa kinara wa upinzani Brian Mundubile, mshirika wa zamani wa rais Edgar Lungu, anayeungwa mkono na muungano wa vyama pinzani, yumo pia Harry Kalaba aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Zambia chini ya utawala wa Lungu.
Wapiga kura milioni 8 na laki 7 wamejiandikisha kushiriki zoezi hilo wengi wao wakiwa wanawake, ambapo wataamua kama mageuzi ya kiuchumi ya Hichilema yanastahili muhula mwingine au ni zamu ya upinzani.
Hichilema, kiongozi wa Chama cha United Party for National Development (UPND), alishinda urais mwaka wa 2021 katika jaribio lake la sita, akirithi nchi ambayo haikuwa na uhuru baada ya miaka mingi ya kukopa chini ya Lungu.
Hata hivyo licha ya kufanikiwa kuiondoa nchi hiyo kwenye mdororo wa kiuchumi, mwanasiasa huyo anashutumiwa kukandamiza wapinzani wake na kushindwa kutekeleza mabadiliko makubwa aliyoahidi, licha ya kwamba bado anapewa nafasi kushinda kwa muhula mwingine.
Disemba mwaka jana 2025 Bunge la Zambia lilipasisha kwa wingi wa kura mswaada wa kurekebisha vifungu vya katiba vinavyohusiana na uchaguzi ambavyo upinzani ulidai vitamsaidia Rais Hakainde Hichilema katika uchaguzi wa mwaka huu.
Zaidi ya asilimia 64 ya wakazi wa Zambia, nchi yenye utajiri wa madini ya shaba, wanaishi katika hali ya umaskini.