Mkurugenzi wa zamani wa UN: Netanyahu na wenzake lazima watiwe mbaroni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141716-mkurugenzi_wa_zamani_wa_un_netanyahu_na_wenzake_lazima_watiwe_mbaroni
Mkurugenzi mmoja wa zamani wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, hawezi kujificha nyuma ya Trump milele; yeye na washirika wake lazima watiwe mbaroni.
(last modified 2026-09-25T09:42:29+00:00 )
Sep 25, 2026 09:12 UTC
  • Mkurugenzi wa zamani wa UN: Netanyahu na wenzake lazima watiwe mbaroni

Mkurugenzi mmoja wa zamani wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, hawezi kujificha nyuma ya Trump milele; yeye na washirika wake lazima watiwe mbaroni.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Craig Mokhiber — aliyekuwa mkurugenzi wa Ofisi ya New York ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa — amesema hayo kujibu hotuba ya Netanyahu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambayo ilisusiwa na sehemu kubwa ya wajumbe wa baraza hilo akabaki anahutubia viti vitupu kwamba: "Kiongozi wa utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid) wa Israel, ambaye anasakwa kwa kesi za kutenda jinai dhidi ya binadamu, ameruhusiwa kuingia Marekani bila ya kukamatwa na kuhutubia Baraza Kuu la UN."

Mokhiber amesema: "Alipopanda jukwaani, kwa mara nyingine tena alisusiwa na mataifa mbalimbali duniani yaliyoonesha kuchukizwa mno na jinai zake. Kama ilivyo kawaida, utawala huo ulileta wafuasi wengi wa Kizayuni kujaza viti vitupu katika jukwaa la watazamaji ukumbini ili kupiga makofi na kushangilia na kuonesha uungaji mkono kwa utawala huo na kiongozi wake mwenye utata, kwa kupiga mayowe ya kifashisti."

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Netanyahu aliwatukana wajumbe wa Baraza Kuu, alisifu waziwazi uhalifu mwingi wa utawala huo, alijigamba kuhusu mashambulizi ya kigaidi ya utawala huo yaliyotumia vifaa vya mawasiliano (pagers) nchini Lebanon, alirudia propaganda zisizo za kweli za utawala huo kuhusu mauaji ya kimbari, alitetea uvamizi haramu wa Isrel huko Palestina na Syria, alimradi alisema uongo kuanzia mwanzo hadi mwisho tena mfululizo na bila ya kusita. Aliwataja walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali na wabaguzi wakubwa wa rangi kuwa eti ni watu wanaopenda amani na wenye heshima, aliwaita watetezi wa haki za kibinadamu kuwa eti ni wenye chuki dhidi ya Mayahudi (antisemitic), na hata aliwashambulia bila ya aibu raia na maafisa wa Marekani ambao wanapinga jinai za utawala wa Kizayuni.

Afisa huyo wa zamani wa haki za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa aidha amesisitiza kwa kusema: "Mtu huyu, ambaye anahusika moja kwa moja na vurugu, hawezi kujificha nyuma ya Trump milele. Yeye na washirika wake lazima watiwe mbaroni na kufikishwa mbele ya sheria; zaidi ya hayo, Umoja wa Mataifa lazima hatimaye uchukue hatua za kuutenga utawala huu na kuushinikiza uwajibike."