Lango-Bahari la Hormuz halitafunguliwa hadi Masharti ya Iran yatekelezwe
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amezitahadharisha nchi jirani kuwa ni lazima masharti saba yaliyowekwa na Iran yatimizwe kabla ya Lango-Bahari la Hormuz kufunguliwa, akisema: "Mkizuia safari za ndege za Iran, safari za ndege zenu nazo pia zitazuiliwa."
Mohsen Rezaei, mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, akizungumza jana Jumatano kujibu madai yaliyotolewa na Trump pamoja na uwezekano wa kuibuliwa upya vita dhidi ya Iran, amesema: "Trump ametoa kauli isiyo na msingi katika Umoja wa Mataifa. Kwa mtazamo wangu, hotuba hiyo ni mojawapo ya makosa makubwa ya kihistoria ya Trump, kwani amejaribu kujitetea huku akionekana wazi kuwa mtenda-jinai aliyeshindwa."
Meja Jenerali Rezaei amesisitiza: Hotuba ya Trump imelenga kuvutia maoni ya umma duniani, katika hali ambayo hata vyombo vya habari vya Marekani yenyewe havizipi uzito tena hotuba zake na vinajizuia kuzisambaza kwa sababu hazina chochote isipokuwa kuwaletea Wamarekani matatizo na aibu. Huko ni kushindwa kunakotia aibu.
Amesema, Trump na Netanyahu wamebuni aina kali na hatazi zaidi za ugaidi duniani ambazo hazijawahi kushuhudiwa tena, na ambazo zimesababisha vifo vya watoto 25,000 duniani, hasa katika Ukanda wa Gaza. Hivyo, ni nani magaidi hasa, wao au sisi ambao watoto wetu wameuawa shahidi wakiwa shuleni?
Meja Jenerali Rezaei amesema: "Tunaweza kuona dalili za kushindwa huku katika uchaguzi unaokuja wa Marekani kupitia matamshi ya Trump. Sababu iko wazi: Ameisababishia Marekani uharibifu mkubwa kiasi kwamba ameharibu umashuhuri wake mwenyewe pamoja na heshima ya chama chake. Hebu angalia hali ya sasa ya upatikanaji wa mafuta, akiba za kimkakati, na uwezo wa makombora nchini Marekani. Mara kwa mara wao huficha takwimu halisi za watu wao waliouawa au kujeruhiwa."
Kuhusu sababu za ushindi wa Iran katika vita na Marekani, amesema: "Wataalamu wengi duniani wanakiri kuwa Iran imeibuka mshindi katika uwanja huo. Leo, Iran iko katika kilele cha nguvu. Haionekani tena kama ilivyokuwa kabla ya vita hivi; katika suala la mamlaka na maendeleo ya kijeshi, tunashikilia nafasi muhimu na ya juu kimataifa na kikanda."
Rezaei ameongeza kuwa: "Hali ya Iran ni tofauti kabisa na ilivyokuwa huko nyuma. Ingawa wakati mwingine tunaweza kutaja baadhi ya masharti, lakini kimsingi Iran ina masharti saba mahususi ambayo yanapaswa kutekelezwa kivitendo, vinginevyo, Lango-Bahari la Hormuz halitafunguliwa kabisa. Kama nilivyosema awali, ni Wamarekani wenyewe ndio wanachukua hatua zinazopelekea kufungwa kwa lango-bahari hilo."