Iran Yabadilisha Kabisa Mahesabu ya Kijeshi Duniani
Mchambuzi mashuhuri wa masuala ya ulimwengu wa Kiarabu, huku akiashiria uchokozi wa hivi karibuni uliofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kutumia teknolojia na mbinu zake mahususi, imevuruga kabisa uwiano wa kijeshi duniani na kama inavyokiriwa na kusisitizwa na wataalamu wa Marekani, imewasababishia wachokozi hao hasara kubwa za kifedha, kiuchumi, kijeshi na kisiasa.
Abdel Bari Atwan, mchambuzi wa masuala ya ulimwengu wa Kiarabu ameandika makala ya kichambuzi na kitaalamu katika gazeti la Rai al-Youm kuhusu makubaliano ya Riyadh na Washington ya kuiuzia Saudi Arabia ndege za kivita aina ya F-35 za Marekani. Amebainisha kuwa habari za ndege hizo ambazo zina uwezo mkubwa wa kutotambulika wala kuonekana kirahisi kwenye rada zimeakisiwa sana katika vyombo vya habari na magazeti ya nchi za Mashariki ya Kati na Marekani, kutokana na sababu tatu kuu.
Kwanza: Matamshi ya Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Iran, aliyesema: "Kipindi kipya kimeanza ambapo ndege za kivita za adui aina ya F-35 zenye teknolojia ya kutotambuliwa na rada, pamoja na nyingine za kisasa aina ya F-15, zinawindwa na kufuatiliwa."
Pili: Kufichuliwa kwa taarifa zinazohusiana na ununuzi wa Saudi Arabia wa ndege 48 za kivita aina ya F-35 zenye teknolojia ya kutotambulika na rada, zenye thamani ya dola bilioni 24.3.
Tatu: Utayari wa Israel wa kutoa mashinikizo dhidi ya serikali ya Marekani ili kupata mifumo ya kisasa ya makombora na ulinzi wa anga ambayo awali Marekani ilikataa kuiuzia.
Atwan anabainisha kuwa katika kila hatua ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miezi saba iliyopita, silaha na makombora mapya ya Iran yamewashangaza na kuwachanganya Waisraeli na Wamarekani. Kuhusu uuzaji wa ndege za kivita za Marekani aina ya F-35 zenye teknolojia ya kutogundulika kirahisi na rada, kwa Saudi Arabia, Atwan anasema: Kukabidhiwa kwa ndege ya kwanza ya aina hiyo kwa Jeshi la Anga la Saudi Arabia hakutafanyika hadi miaka mitano baada ya makubaliano ya mauazo kusainiwa. Katika kipindi hiki cha miaka mitano, mabadiliko makubwa ya kisiasa na kijeshi yanaweza kutokea katika eneo la Asia Magharibi, ikiwemo uwezekano wa kutokuwepo kabisa kwa vikosi au kambi za Marekani katika eneo, iwe ni kutokana na kuharibiwa kabisa kwa kambi na vituo vyake vya kijeshi au uamuzi wake wa kujiondoa ili kupunguza hasara.
Mchambuzi huyu Mwarabu anaendelea kusema: Hakuna shaka kwamba Marekani ni taifa lenye nguvu kubwa, na kabla ya kuanzisha uchokozi wake dhidi ya Iran, ilikuwa na maghala makubwa zaidi ya akiba ya silaha, ndege za kivita na makombora duniani; hata hivyo, hali hiyo imebadilika kufuatia uchokozi huo, huku ushindi halisi na wa wazi zaidi ukionekana katika mafanikio ya makombora ya balistiki ya Iran katika kushambulia kambi za kijeshi za Marekani katika eneo. Atwan amesisitiza kuwa John Cordell Jenerali mkongwe wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, amethibitisha katika mahojiano na gazeti la Military Times yaliyochapishwa siku tatu zilizopita kwamba kuharibiwa kwa kituo cha usaidizi cha wanamaji wa Marekani huko Manama Bahrain kumekuwa sawa na kupoteza manowari moja ya Marekani inayobeba ndege za kivita. Ujenzi wa kituo kama hicho katika eneo hilo uliigharimu Marekani mamia ya mabilioni ya dola, hivyo kuharibiwa kwake kwa kasi na urahisi wa kiasi hicho kumeiletea nchi hiyo aibu kubwa na kutoa pigo kwa itibari yake ya kimataifa.
Amesema kuwa Iran, ambayo tayari imevunja dhana potofu na uvumi ulioenezwa duniani kwa makusudi ili kuhadaa na kuutisha ulimwengu kuhusu uwezo wa Kihollywood wa makombora ya ulinzi wa anga ya Patriot, pia ina uwezo wa kufuatilia na kutungua ndege za kivita za Marekani zisizoonekana kwenye rada, na tayari imethibitisha kivitendo suala hillo kama tulivyoshuhudia katika vita vya karibuni. Iran imefanikiwa kumaliza akiba ya makombora ya ulinzi wa anga ya Marekani na Israel. Ikiwa Ghalibaf anasema kuwa enzi mpya imeanza ambapo ndege za Marekani aina ya F-15 na F-35 zenye teknolojia ya kutogundulika kirahisi zinawindwa na kufuatiliwa, muamini. Muda utathibitisha ukweli wa maneno yake hivi karibuni.