Bei ya dizeli Marekani na Ulaya yapanda na kuvunja rekodi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141656-bei_ya_dizeli_marekani_na_ulaya_yapanda_na_kuvunja_rekodi
Bei ya dizeli nchini Marekani na katika nchi za Ulaya imefikia viwango vipya vya rekodi, huku changamoto za usambazaji na misukosuko katika soko la nishati zikiendelea kuongeza gharama za mafuta.
(last modified 2026-09-23T03:57:45+00:00 )
Sep 23, 2026 03:56 UTC
  • Bei ya dizeli Marekani na Ulaya yapanda na kuvunja rekodi

Bei ya dizeli nchini Marekani na katika nchi za Ulaya imefikia viwango vipya vya rekodi, huku changamoto za usambazaji na misukosuko katika soko la nishati zikiendelea kuongeza gharama za mafuta.

Kuendelea mgogoro wa Asia Magharibi na hali ya Mlango Bahari wa Hormuz kumesababisha bei ya dizeli nchini Marekani na Ulaya kufikia viwango vya juu visivyowahi kurekodiwa.

Jarida la OilPrice liliandikka katika toleo lake la jana Jumanne, kwamba bei ya dizeli nchini Marekani ilivunja tena rekodi wiki iliyopita, baada ya kuvuka dola 6.50 kwa kila galoni. Ulaya pia, bei ya mafuta imepanda kwa kiwango kikubwa, huku hofu ya upungufu wa mafuta ikiendelea kuathiri uchumi ambao tayari unakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Uwezo wa vituo vya kusafisha mafuta duniani hautoshi kufidia kupungua kwa usambazaji wa mafuta ghafi na bidhaa za petroli kutoka Mashariki ya Kati na Ruussia huku kukiwa hakuna suluhisho la haraka kwa hali hiyo.

Russia ilitangaza wiki iliyopita kwamba itaongeza muda wa marufuku ya kuuza nje dizeli hadi mwishoni mwa mwezi Oktoba, wakati mashambulizi ya ndege zisizo na rubani ya Ukraine dhidi ya vituo vya kusafisha mafuta vya Russia yakiendelea.

Mashambulizi hayo yanaendelea licha ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuitaka serikali ya Volodymyr Zelensky kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati. Trump amehusisha kupanda bei ya dizeli na mashambulizi hayo pekee. Katika shambulio la hivi karibuni, lililofanyika Jumapili, moja ya vituo vikubwa zaidi vya kusafisha mafuta nchini Russia kililengwa.

Mbali na dizeli, bidhaa azingine za nishati kama petrol pia zinaonekana kuvunja rekodi ya bei katika mataifa mengi ya Ulaya. Kabla ya Marekani na Israel kuivamia kijeshi Iran, hali ya nishati haikuwa nzito kiasi hiki duniani.