IRGC: Ukianzishwa uchokozi mpya, jiografia ya vita na silaha itakazotumia Iran vitabadilika
Shambulio lolote jipya dhidi ya Iran litasababisha mabadiliko makubwa katika jiografia ya vita na aina ya silaha zitakazotumika. Hayo yameelezwa na msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
"Iwapo kutatokea uchokozi mwingine, bila shaka kutakuwa na mabadiliko makubwa katika mfumo wetu wa ulinzi na hatua zetu za kujibu mashambulizi," ameeleza Brigedia Jenerali wa Daraja la Pili Hossein Mohebbi na kusisitiza: "ni hakika kwamba tutaibadilisha jiografia ya vita."
Amesema Iran itaanza kutumia silaha na zana mpya za kijeshi zenye uwezo mpya, na kuongeza kuwa "dunia itashangazwa" nazo.
Aidha, Brigedia Jenerali Mohebbi ametaja maeneo kadhaa ambayo Marekani imepata vipigo vya kushindwa kimkakati katika vita vyake ilivyoanzisha bila sababu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
"Marekani imeshindwa katika vita hivi, na kushindwa kwake ni kwa kiwango cha kihistoria na cha udhalilishwaji, lakini haina ujasiri wa kukiri na kukubali kushindwa huko," ameeleza msemaji wa IRGC.
Mohebbi amesema, Washington imeshindwa kuufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, licha ya kumiliki jeshi kubwa zaidi la majini duniani na huku ikiwa inadai kwamba, moja ya sababu kuu za uwepo wake katika eneo hilo na duniani kote ni kuhakikisha usalama wa nishati na uhuru wa safari za vyombo vya majini.
"Moja ya maeneo ambayo Marekani imeshindwa ni kufeli kwake kuufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz," amesema Brigedia Jenerali Mohebbi na kuongeza kuwa Washington ilitumia uwezo wake wote lakini "haikuweza" kufungua njia hiyo ya majin baada ya Iran kuifunga ikiwa ni hatua ya kujibu uchokozi wa kijeshi wa pamoja uliofanywa na Marekani na Israel.
Msemaji wa IRGC amezitaja pia kambi za kijeshi za Marekani katika eneo kama mzigo mwingine kwa Washington.
"Kushindwa kwa Marekani hapa kulitokana na ukweli kwamba uwekezaji wake wote wa kuimarisha usalama uligeuka kuwa kinyume chake," ameeleza Mohebi na kuongeza kuwa kambi hizo zilikumbwa na mashambulizi makali ya Vikosi vya Majeshi ya Iran.
Amekutaja kushindwa kukubwa kwa Marekani kuwa ni katika uga wa intelijensia na ujasusi na kubainisha kwamba, Washington imekuwa ikionekana kuwa na umiliki wa mfumo wa hali ya juu na usiotasawirika wa intelijensia unaolindwa na teknolojia za kisasa kabisa.
Hata hivyo, amesema, makombora ya Iran yalivishambulia vituo vya intelijensia na ujasusi vya Marekani katika maeneo yanayozunguka Ghuba ya Uajemi na kaskazini mwa Iraq, jambo lililoonyesha kuwa vituo hivyo havikuwa nje ya uwezo wa kutoweza kufikiwa.
Mohebbi amesema Iran iliweza kuvifuatilia na kuvitambua vituo hivyo na kuvishambulia, hatua iliyoashiria "kushindwa kukubwa kiintelijinsia" kwa Marekani mbele ya wapinzani na washirika wake.
"Haya yote ni tofauti na kule kushindwa kulifikia lengo," ameeleza Mohebbi na kuongeza kuwa kushindwa huko kuna maana ya kushindwa kimkakati…/