China yaionya vikali Marekani, msithubutu...!
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141704-china_yaionya_vikali_marekani_msithubutu...!
Wizara ya Ulinzi ya China imetoa onyo kali kwa Marekani ikiitaka isithubutu kuiuzia silaha Taiwan.
(last modified 2026-09-25T03:32:10+00:00 )
Sep 25, 2026 03:31 UTC
  • China yaionya vikali Marekani, msithubutu...!
    China yaionya vikali Marekani, msithubutu...!

Wizara ya Ulinzi ya China imetoa onyo kali kwa Marekani ikiitaka isithubutu kuiuzia silaha Taiwan.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al-Mayadeen, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China, Jiang Pin alisema jana Alkhamisi kwamba, lazima Washington ijihadhari sana katika maamuzi yake ya kuiuzia silaha Taiwan. Kauli hiyo ilitolewa muda mfupi kabla ya mkutano wa kilele kati ya Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Marekani Donald Trump, mjini Washington.

Msemaji huyo wa Wizara ya Ulinzi ya China ameongeza kwa kusema: "Ni lazima tusisitize kuwa Taiwan ndilo suala muhimu zaidi katika uhusiano kati ya China na Marekani, na kwamba kudumisha amani na utulivu katika Lango-Bahari la Taiwan kunapaswa kuwa ndiyo maslahi makuu ya pamoja kati ya nchi hizo mbili."

Mwezi Disemba mwaka jana, serikali ya Trump iliidhinisha makubaliano ya kuipa Taiwan silaha zenye thamani ya dola bilioni 11. Hayo yalikuwa ni makubaliano makubwa zaidi ya aina yake. Hata hivyo, makubaliano ya pili yenye thamani ya takriban dola bilioni 14 yamekwama kwa miezi kadhaa.

Mwezi Mei mwaka huu pia Rais wa China alionya katika mazungumzo yake na rais mwenzake wa Marekani, Donald Trump huko Beijing kwamba: Kosa lolote la Washingto la kuipa silaha Taiwan linaweza kusababisha mzozo mkubwa kati ya nchi hizo mbili.

China inaitambua Taiwan kuwa ni sehemu isiyoweza kutenganishwa ya Jamhuri ya Watu wa China na inalitaja suala la kufuata "kanuni ya China Moja" kama sharti muhimu kwa nchi zinazotaka kuanzisha au kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na China.