Marekani: Nguvu Kubwa Kidhahiri, Lakini Tupu kwa Ndani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141638-marekani_nguvu_kubwa_kidhahiri_lakini_tupu_kwa_ndani
Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Iran, akizungumzia hali halisi ya Marekani, amesema: "Kinyume na muonekano wake wa nje, Marekani iko katika hali ya udhaifu na hatari kubwa."
(last modified 2026-09-22T11:12:12+00:00 )
Sep 22, 2026 11:07 UTC
  • Marekani: Nguvu Kubwa Kidhahiri, Lakini Tupu kwa Ndani

Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Iran, akizungumzia hali halisi ya Marekani, amesema: "Kinyume na muonekano wake wa nje, Marekani iko katika hali ya udhaifu na hatari kubwa."

Taasisi kubwa ya kibenki ya JPMorgan hivi karibuni ilianza kuwasilisha ripoti yake ya kila wiki ya utabiri wa soko la mafuta kwa kauli isiyotarajiwa: "Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita na Iran, hatuna ruwaza ya msingi. Kwa kweli hatujui namna ya kubuni mfano au kutabiri matokeo ya mwisho ya hali hii."

Kufuatia msimamo huu usio wa kawaida uliochukuliwa na wachambuzi wakuu wa masoko ya fedha, Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bungem la Iran, ameandika kwenye ukurasa wake binafsi wa X kwamba: 'Hali hii inafanana kabisa na kitendawili cha Schrödinger: Utawala wa Marekani ni kama kabati la Schrödinger lililojaa sahani ambazo ziko hatarini kuanguka. Kwa nje, inaonyesha taswira ya utawala ulio na udhibiti na nguvu kubwa, lakini kwa kiuhalisia, iko katika hatari na udhaifu mkubwa. Inajaribu kuibana Iran na kutarajia kutokabiliwa na madhara yoyote, jambo ambalo haliwezekani kabisa.'

Akiashiria msimamo usio wa kawaida wa wachambuzi wa JPMorgan ambao, kwa mara ya kwanza tangu vita na Iran vianze, wamesema hawana msingi wowote wa kutabiri mwenendo wa soko la mafuta, Ghalibaf amelinganisha hali ya sasa ya Marekani na "kitendawili cha Schrödinger": Kabati lenye sahani nyingi zinazoonekana kuwa salama lakini ziko katika hali tata tayari kuanguka na kuvunjika, ambapo kufunguliwa mlango wa kabati hilo kunasababisha zote kudondoka na kuvunjika. Mtazamo huu unaakisi hali halisi ya sasa ya Marekani: Taifa ambalo kwa nje linaonyesha taswira ya udhibiti mkubwa wa mambo na ubora wa juu, lakini kiuhalisia, liko katika hatari kubwa na ukingoni mwa mporomoko. Taswira hii ya kimafumbo inatokana na uhalisia ambao umedhoofisha mfumo wa nguvu wa Marekani kutokea ndani.

Katika mtazamo wa uchumi, takwimu rasmi zinaonyesha kiwango cha kudhoofika huku. Kufikia Septemba hii, jumla ya deni la taifa la Marekani lilikuwa limevuka kiwango cha dola trilioni 40, huku deni la umma likifikia dola trilioni 32.42. Uwiano wa deni la serikali kuu mkabala wa Pato la Taifa (GDP) umefikia takriban asilimia 101 na unatarajiwa kupanda hadi asilimia 120 kufikia mwaka 2036. Malipo ya riba pekee yamekuwa kipengele cha tatu kwa ukubwa katika bajeti ya serikali kuu, yakifikia dola bilioni 529 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.

Wakati huo huo, pengo la utajiri limefikia viwango visivyopata kushuhudiwa: Sehemu ya mapato ya taifa inayokwenda kwa wafanyakazi kama mishahara na marupurupu imeshuka hadi kiwango cha chini kabisa tangu miaka ya 1950, huku faida za makampuni zikifikia kilele cha juu zaidi tangu Vita vya Pili vya Dunia. Asilimia moja ya watu matajiri zaidi nchini Marekani wanamiliki karibu asilimia 30 ya utajiri wote wa taifa, huku nusu ya jamii iliyo na kipato cha chini ikimiliki juu kidogo ya asilimia 5 tu. Hali hii ya kiuchumi inaonyesha kuwa matunda ya ukuaji wa uchumi yanawanufaisha wale walio katika tabaka la juu pekee, huku yakizidi kuinyima sehemu nyingine ya jamii utajiri wao halali. Kudhoofika huku pia kunaonekana katika nyanja za kijamii na kisiasa. Kwa mujibu wa tathmini ya Jumuiya ya Wahandisi wa Kiraia ya Marekani, miundombinu muhimu ya Marekani imepokea daraja la "C" pekee, ambapo kutodhaminiwa usambazaji thabiti wa umeme na mitandao ya mawasiliano yenye kasi kubwa kumeviibulia viwanda vya Marekani changamoto na vikwazo vikubwa. Katika maadhimisho ya miaka 250 ya uhuru wa taifa, kwa uchache majimbo saba yamekataa kushiriki katika maonyesho ya kitaifa ya "Marekani Kuu", ambapo wachambuzi wanaashiria "mgawanyiko mkubwa" na kupungua kwa imani ya umma kwa taasisi za kisiasa, mambo ambayo yamedhoofisha uwezo wa Washington wa kuthibitisha madai yake ya kutawala dunia. Migawanyiko hii inaonyesha kwamba "Kabati la Schrödinger" limeanza kuonyesha ishara za kuporomoka si kwa nje tu bali pia kutokea ndani. Kwa mtazamo wa kimkakati na kijeshi, uzoefu wa Afghanistan na matokeo yake vinaonyesha wazi mipaka ya nguvu ya Marekani. Ni vita vya miaka ishirini vilivyogharimu dola trilioni 2.26 na kuhusisha kutumwa nchini humo zaidi ya askari 77,000 wa Marekani, huku vikiacha takriban watu 2,500 wakiwa wamepoteza maisha. Ni vita ambavyo hatimaye vilipelekea Taliban kurejea madarakani na kutajwa kuwa "kushindwa kubaya sana kwa Marekani."

Sasa, kuhusu Iran, JPMorgan imekiri kuwa hata haijui namna ya kubuni mfano wa kutabiri "hatua ya mwisho" ya vita vinavyoendelea, kwani mipaka yote muhimu ya kiuchumi imevukwa, ambapo bei ya mafuta ghafi imezidi dola 100, bei ya petroli imekaribia dola 5 kwa galoni, na riba ya dhamana za serikali imezidi asilimia 5, na bado hakuna mkakati wowote wa wazi uliowasilishwa kwa ajili ya kujiondoa kwenye hali hiyo. Kwa kutumia vizuri uwezo wake wa kipekee na usiowiana na ule wa adui katika nyanja za makombora, ndege zisizo na rubani, na mtandao (cyberspace), Iran imefanikiwa katika kuibebesha Marekani gharama kubwa za vita na kufanya udhibiti wa Lango-Bahari la Hormuz kuwa wenzo wake muhimu wa kimkakati. Mwanahistoria mwenye msimamo wa kihafidhina mamboleo (neoconservative), Robert Kagan, pia amekiri kuwa vita hivi vinaweza kuwa vinaashiria kuporomoka kwa utawala wa Marekani, kuporomoka ambako, tofauti na changamoto zilizopita, hakuwezi kurekebishika wala kupuuzwa. Hivyo, taswira ya "sahani za Schrödinger" iliyotumiwa na Ghalibaf, ni sitiara mwafaka inayoelezea hali ya sasa ya Marekani. Ni taifa linaloonekana kuwa imara na lenye nguvu kubwa kwa nje, lakini lipo ukingoni mwa kuporomoka kutokana na mzigo mkubwa wa madeni, pengo linalozidi kuongezeka kati ya matabaka ya kijamii, miundombinu inayochakaa, mgawanyiko mkubwa wa kisiasa na mkwamo wa kimkakati katika Mashariki ya Kati. Kama ambavyo JPMorgan haiwezi kutabiri matokeo ya mwisho ya hali hii, mifumo ya kawaida ya kuainisha nguvu za kitaifa nayo imeshindwa kutegua kitendawili hiki. Kilicho dhahiri ni kwamba Iran ndiyo inayoshikilia mpini wa kabati hilo, ambapo Marekani inapaswa kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu wakati wa kufunguliwa mlango wa kabati hilo.