Afrika Kusini yalaani mpango wa Marekani wa kuwapa upendeleo Makaburu
-
Trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, amelaani vikali mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kuwapa hifadhi Waafrikaner, yaani Makaburi ambao ni kikundi cha wachache wenye asili ya Kizungu nchini Afrika Kusini, akiutaja mpango huo kama “Apathaidi ya Awamu ya Pili.”
Lamola ametoa kauli hizo katika Jukwaa la Diaspora ya Afrika jijini Washington.
Waziri huyo amebainisha kuwa mpango huo unatoa upendeleo kwa wazungu wa Afrika Kusini huku ukiwabagua watu wa makabila mengine.
Alisema: “Ni Waafrikaner wazungu pekee kutoka Afrika Kusini ndio wanaoruhusiwa kuwa wakimbizi hapa. Na nyinyi nyote au mtu yeyote wa rangi nyingine haruhusiwi. Hii ni sera yenye misingi ya ubaguzi wa rangi, ambayo sisi tunaiita Apathaidi ya Awamu ya Pili.”
Waafrikaner au Makaburu ni kundi la kikabila linalozungumza Kiafrikana na lenye asili ya Kizungu, wakitokana na walowezi kutoka Uholanzi, Ujerumani, na Ufaransa walioanza kuwasili kusini mwa Afrika katika karne ya 17. Serikali zilizokuwa zikiongozwa na Waafrikaner ziliasisi mfumo ubaguzi wa rangi (apartheid), mfumo wa utengano wa kirangi uliomalizika mwaka 1994.
Trump alianzisha mpango huo wa kuwapa hifadhi Makaburu kupitia amri ya kiutendaji aliyoitia saini Februari 2025, akidai kuwa wanakabiliwa na ubaguzi wa rangi unaofadhiliwa na serikali, vurugu, na kutaifishwa kwa ardhi chini ya Sheria ya Kutaifisha Ardhi (Expropriation Act) ya Afrika Kusini.
Pretoria imeyatupilia mbali madai hayo, ikisisitiza kuwa sheria hiyo imelenga kushughulikia ukosefu wa usawa katika umiliki wa ardhi uliorithiwa kutoka kipindi cha utawala wa kubaguzi wa Makaburu, na kwamba hakuna mali ya watu binafsi iliyotaifishwa chini ya sheria hiyo.
Trump alipanua mpango huo mnamo Mei 2026, akiongeza idadi ya wakimbizi wanaokubaliwa nchini Marekani kila mwaka kutoka 7,500 hadi 17,500 na kutenga nafasi hizo za ziada kwa ajili ya Waafrikaner pekee, akidai kuwepo kwa “hali ya dharura isiyotarajiwa ya wakimbizi.”