Baghaei: Usalama hautorejea Hormuz madhali Marekani inaendeleza vita
-
Esmaeil Baghaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa: "Usalama hautorejea katika Lango-Bahari La Hormuz madhali Marekani inaendeleza vita."
Esmaeil Baghaei amesema hayo wakati alipokuwa anajibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano wake wa kila wiki na vyombo vya habari jana Jumatatu hapa Tehran.
Mwanzoni mwa mkutano huo ametoa salamu za rambirambi baada ya magenge ya kigaidi yanayoongozwa na Marekani, Israel na vibaraka wako kwenye eneo hili, kumuua shahidi afisa mmoja wa kulinda usalama wa taifa katika mkoa wa Sistan na Baluchestan nchini Iran kwa kusema: "Ninatoa rambirambi zangu kwa watu watukufu na wenye heshima wa Sistan na Baluchestan kufuatia kuuawa shahidi afisa huyo. Ameuawa shahidi katika shambulio la kigaidi na alikuwa na shahada ya uzamivu (PhD) katika Teknolojia ya Habari (IT). Tunazienzi roho za mashahidi wote wa Iran."
Akijibu matamshi ya uchochezi dhidi ya Iran yaliyotolewa na Marco Rubio waziri wa mambo ya nje wa utawala wa kigaidi wa Marekani, msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Hotuba ya Rubio na namna alivyowasilisha hoja zake lazima ihesabiwe kuwa ni sehemu ya vita vya Marekani vya kushambulia fikra za walio wengine duniani ili kuzifanya ziwe na mtazamo mbaya kuhusu Iran."
Amesema: "Kuwasilisha tafsiri potofu kwa lengo la kuhalalisha uchochezi wa vita wa Marekani ni matusi kwa ustaarabu wa Iran. Bila ya kuelewa, waziri wa mambo ya nje wa Marekani amekiri ukweli kwamba Iran imedumu kwa maelfu ya miaka, na kwamba kustawi, kukuwa na kuendelea kuwepo ustaarabu mkongwe kama wa Iran hakutokani na mashambulizi na uvamizi wa kijeshi."
Amesema: "Siri ya mafanikio haya kudumu ya Iran iko katika uwazi wake wa kushirikiana na wengine. Hatujawahi kutumia mbinu ya kuwakataa au kuwafuta wengine kama njia ya kudumisha ustaarabu na utamaduni wetu."