Msumbiji yaweka tarehe ya mwisho kusalimisha silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i142148-msumbiji_yaweka_tarehe_ya_mwisho_kusalimisha_silaha_zinazomilikiwa_kinyume_cha_sheria
Rais wa Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, ameonya kwamba silaha zote zinazomilikiwa kinyume cha sheria zitapokonywa baada ya mwezi Desemba, tarehe ya mwisho ya kumalizika kwa mpango wa msamaha wa polisi.
(last modified 2026-10-13T03:44:18+00:00 )
Oct 13, 2026 03:41 UTC
  • Rais wa Msumbiji, Daniel Francisco Chapo
    Rais wa Msumbiji, Daniel Francisco Chapo

Rais wa Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, ameonya kwamba silaha zote zinazomilikiwa kinyume cha sheria zitapokonywa baada ya mwezi Desemba, tarehe ya mwisho ya kumalizika kwa mpango wa msamaha wa polisi.

Rais Chapo alifafanua kwamba raia wangesalimisha silaha zao kabla ya tarehe hiyo bila kuhojiwa, kuadhibiwa, au kukamatwa.

Akizungumza katika sherehe za kufunga mafunzo ya operesheni maalum, Rais wa Msumbiji  amehimiza jeshi la polisi kuonyesha nidhamu, taaluma na kuheshimu sheria ili kudumisha usalama na utulivu wa umma.

"Utaalamu hauwaweki ninyi juu ya sheria. Kinyume chake, kadiri uwezo wa kioperesheni wa kikosi unavyokuwa mkubwa, ndivyo nidhamu yake inavyopaswa kuwa thabiti zaidi," alisema, akibainisha kwamba, utumiaji wa mamlaka lazima uheshimu haki za binadamu na uhuru wa kimsingi wa raia.

Chapo pia alitetea uwekezaji endelevu katika mafunzo ya polisi. Alibainisha kwamba usalama wa umma ni muhimu kwa kufikia uhuru wa kiuchumi, kuhifadhi amani, kutetea uhuru wa taifa, na kulinda uadilifu wa eneo.

Kutokana na kuongezeka kwa ugumu wa uhalifu, hasa biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya, utekaji nyara, uhalifu uliopangwa na uhalifu wa kimtandao, Chapo amesisitiza haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya jeshi la polisi na vikosi vingine vya ulinzi na usalama ili kuboresha majibu ya tishio hilo.

Mkoa wa kaskazini mwa Msumbiji wa Cabo Delgado umekuwa ukikumbwa na uasi wa makundi ya kigaidi tangu mwaka 2017. Chapo alisema kwamba hali imeimarika katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na juhudi za vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo, pamoja na wanajeshi wa Rwanda na Tanzania, katika mapambano dhidi ya ugaidi.