Trump sasa amgeuka rasmi Zelenskyy, aitaka Ukraine itafute rais mwingine mpya
Rais wa Marekani Donald Trump ameitaka Ukraine imuondoe madarakani Volodymyr Zelenskyy, na kutafuta rais mwingine mpya, akimkasirikia rais huyo wa Ukraine kwa sababu ya mashambulio yanayofanywa dhidi ya viwanda vya kusafisha mafuta vya Russia, ambayo amesema yamechangia kupanda kwa bei ya dizeli duniani.
Trump alitoa lawama hizo kali siku ya Jumamosi huku uhusiano kati ya Marekani na Ukraine ukiharibika kutokana na makubaliano ya usambazaji wa dizeli aliyofikia rais huyo wa Marekani na mwenzake wa Russia.
Kupanda kwa kasi bei ya dizeli duniani, kufuatia kuzuka kwa vita vya Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, kumekibebesha dhima nzito ya kisiasa chama cha Trump cha Republican kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika nchini Marekani mwezi ujao, huku kukiwa na uwezekano wa mrengo wa upinzani wa Wademocrat kudhibiti moja au mabaraza yote mawili ya bunge la nchi hiyo, Congress.
"Nadhani ni wakati wa Ukraine kupata rais mpya," Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, akisema Zelenskyy ameharibu vifaa vya dizeli duniani kwa mashambulio yaliyolenga viwanda vya kusafisha mafuta vya Russia.
"Anataka kuwasababishia matatizo wakulima wetu na wafugaji wetu ya mafuta ya dizeli kwa sababu Russia inatoa sehemu kubwa ya mafuta ya dizeli duniani kote", aliendelea kueleza Trump.
Hata hivyo, Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Andrii Sybiha amemtetea Zelenskyy na kumjibu rais wa Marekani kupitia andiko aliloweka kwenye mtandao wa X akisema:
"Yeye anaungwa mkono na watu wa Ukraine, na wao wana haki ya kuamua".
Sybiha ameongezea kwa kusema: "kauli zinazotoka nje zinathibitisha tu kwamba anafanya kazi yake vizuri. Anastahili kuungwa mkono."
Trump, ambaye kwa wiki kadhaa amekuwa akimsihi Zelenskyy aache kushambulia miundombinu ya nishati ya Russia, alifikia makubaliano na Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin siku ya Ijumaa ya kununua dizeli kutoka Russia katika jitihada za kupunguza bei inayopaa ya mafuta.
Makubaliano hayo yaliashiria mabadiliko makubwa na ya kushangaza katika msimamo wa miaka mingi wa Washington wa kuiwekea mashinikizo Russia kuhusiana na vita vyake na Ukraine.
Trump ametaka kuibebesha lawama Ukraine ya kupanda bei ya dizeli ya ndani ya Marekani badala ya vita ilivyoanzisha Marekani na utawala wa kizayuni dhidi ya Iran, ambavyo ndivyo hasa vilivyosababisha kupanda bei ya nishati duniani…/