Ghalibaf aiambia Marekani: Mtawapigia magoti Wairani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i142090-ghalibaf_aiambia_marekani_mtawapigia_magoti_wairani
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amemjibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani kwa kumwambia: "Wale wanaotafuta urithi wa Alexander watakumbwa na hatima ya Valerian; mtapiga magoti!"
(last modified 2026-10-10T11:48:17+00:00 )
Oct 10, 2026 11:47 UTC
  • Ghalibaf aiambia Marekani: Mtawapigia magoti Wairani

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amemjibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani kwa kumwambia: "Wale wanaotafuta urithi wa Alexander watakumbwa na hatima ya Valerian; mtapiga magoti!"

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Mohammad Bagher Ghalibaf ametumia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii kujibu bwabwaja za hivi karibuni na zisizo na msingi za waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Marco Rubio, kuhusu ustaarabu wa Iran na kuandika: "Katika historia yote, sisi Wairani tumepambana vilivyo na wale waliojitangaza kuwa ni mabwana wa dunia na kujaribu kufuta staarabu za kale katika uso wa dunia."

Aidha ameandika: "Walikuja na moto na miali mikali, lakini waliondoka wakiwa mavumbini na kwa aibu."

Spika Ghalibaf ameongeza kuwa: "Wale wanaotafuta urithi wa Alexander watakumbwa na hatima ya Valerian; mtawapigia magoti Wairani."

Kabla ya hapo pia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa amesema kwamba Iran haitolifungua Lango-Bahari la Hormuz hadi masharti saba yaliyowekwa na Tehran, kwa mujibu wa makubaliano ya Islamabad, yatakapotekelezwa.

Kwa upande wake, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH), ametoa onyo akisema kuwa jeshi hilo liko tayari kutoa jibu kali kwa hatua yoyote ya kimakosa ya adui katika mahesabu yake.

Meja Jenerali Ahmad Vahidi alisema hayo katika ujumbe wake wa kuadhimisha tarehe 8 Oktoba, Siku ya Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba, Iran itajibu kwa nguvu tishio lolote katika Lango-Bahari la Hormuz.

Meja Jenerali Ahmad Vahidi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, vilevile alisema Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi (SEPAH) lina uwezo mkubwa na linafanya kazi kwa uratibu wa karibu na Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.