CNN: Vita vya Iran vaisababishia Marekani hasara ya dola bilioni 3.3
-
CNN: Vita vya Iran vaisababishia Marekani hasara ya dola bilioni 3.3
Televisheni ya CNN ya Marekani ambayo ni moja ya televisheni kubwa na za daraja la kwanza nchini humo imetangaza kuwa, vita vilivyoanzishwa na Washington dhidi ya Iran tarehe 28 Februari 2026 vimeisababishia Marekani hasara ya takriban dola bilioni 3.3.
Katika ripoti yake ya kiutafiti na kwa kutegemea ripoti ya Bunge la Marekani, televisheni hiyo ya CNN imethibitisha kuwa jeshi la nchi hiyo limepoteza ndege za kivita, helikopta, na ndege zisizo na rubani (droni) 81, zenye thamani ya takriban dola bilioni 3.3 wakati wa vita dhidi ya Iran.
Televisheni hiyo imefuatilia taarifa ya "New York Post" iliyonukuu taarifa ya Kitengo cha Utafiti wa Bunge (CRS) ikiripoti kuwa, jeshi la Marekani lilipoteza ndege za kivita, helikopta na droni 81 ambazo ima zimeharibiwa kabisa au kuharibika sehemu fulani, katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya Marekani.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, thamani ya ndege zilizopotea za jeshi la Marekani katika vita dhidi ya Iran haipungui dola bilioni 3.3 na kiwango hicho ni cha vifaa tu vilivyotajwa hapo juu vya jeshi la Marekani bila ya kuzingatia hasara nyinginezo za roho za watu, majengo, kambi za kijeshi, kufichuka taarifa muhimu za silaha za Marekani, n.k.
Ripoti hiyo ya CNN ambayo kimsingi imetegemea takwimu kutoka Pentagon na kutoka kwa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Idara ya Vita ya nchi hiyo inaonesha ukubwa wa hasara iliyopata Washington baada ya zaidi ya miezi saba ya tangu kuanzisha kwake vita vya kichokozi dhidi ya Iran.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa hasara kiliyopata kikosi cha anga cha Marekani wakati wa operesheni za kijeshi dhidi ya Iran inajumuisha baadhi ya ndege za kisasa zaidi za nchi hiyo.
Sehemu nyingine ya ripoti hiyo ya CNN imehusiana na Marekani kupoteza kwa uchache droni 45 aina ya "MQ-9 Reaper"; thamani ya kila moja inakadiriwa kuwa ni kati ya dola milioni 30 hadi milioni 50. Pia Marekani imepoteza ndege 12 za kivita aina ya F-15E Strike Eagle, ndege kadhaa za KC-135 za kuongeza mafuta angani na kwa uchache ndege moja aina ya F-35A.
Kitengo cha Utafiti cha Bunge la Marekani kimesema pia kuwa, takwimu hizo zinaweza kubadilika na hasara kuwa kubwa zaidi kutokana na usiri na uchujaji mkubwa wa baadhi ya taarifa, operesheni za kijeshi na masuala mengine kama hayo.