Rais Pezeshkian amwambia Putin: Iran haitajiondoa kwenye meza ya mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i142064-rais_pezeshkian_amwambia_putin_iran_haitajiondoa_kwenye_meza_ya_mazungumzo
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza tena dhamira ya Tehran ya kutatua masuala kupitia diplomasia, huku akipinga vikali hatua za upande mmoja za Marekani.
(last modified 2026-10-09T09:51:34+00:00 )
Oct 09, 2026 09:50 UTC
  • Rais Pezeshkian amwambia Putin: Iran haitajiondoa kwenye meza ya mazungumzo
    Rais Pezeshkian amwambia Putin: Iran haitajiondoa kwenye meza ya mazungumzo

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza tena dhamira ya Tehran ya kutatua masuala kupitia diplomasia, huku akipinga vikali hatua za upande mmoja za Marekani.

Rais Pezeshkian amesema hayo katika mazungumzo yake na Rais Vladimir Putin wa Russia pambizoni mwa mwa mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Huru (Commonwealth of Independent States) CIS kwa kifupi na mkutano kuhusu masuala ya mazingira ya Bahari ya Caspian, mjini Turkmenbashy Turkmenistan ambapo amesisitiza kuwa,  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitajiondoa kwenye meza ya mazungumzo, licha ya Marekani kuendelea na mashambulizi yake.

“Tunashiriki katika mazungumzo ya kidiplomasia; hata hivyo, kila tunapozungumza na Marekani, wao huanzisha mashambulizi mapya. Licha ya hayo, hatutajiondoa kwenye meza ya mazungumzo,” amesema Rais Pezeshkian.

Dakta Pezeshkian amesema: “kumefanyika mabadilishano ya mapendekezo kati ya upande wetu na Wamarekani, nasi tumefanya marekebisho yetu wenyewe kwa mapendekezo hayo. Mara tu yatakapokamilishwa, tunakusudia kukaa pamoja na wapatanishi husika ili kuyaunganisha na kuhitimisha suala hili.”

Pezeshkian ameipongeza Moscow kwa msimamo wake wa kudumu wa kupinga hatua za upande mmoja, akiongeza kuwa Iran nayo inafuata njia hiyo hiyo.

Aidha, ameishukuru Russia kwa misimamo yake katika masuala ya kikanda na ndani ya Umoja wa Mataifa, pamoja na mchango wake katika kukabiliana na hatua za upande mmoja zinazochukuliwa bila kudhibitiwa.

Aidha katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Armenia, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa kuimarisha imani ya pande zote na kupanua ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Akiashiria kuwa nchi hizo mbili ni majirani na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano na maingiliano, amesema kuwa Iran na Armenia, kama nchi jirani, zinapaswa kuwa na uwezo wa kushirikiana na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kudumisha uthabiti katika mahusiano ya pande mbili, na kutangaza utayari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kupanua ushirikiano na Armenia katika nyanja mbalimbali.