Askari wa US waliojeruhiwa katika shambulio la Iran wasema jeshi limewatelekeza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i142026-askari_wa_us_waliojeruhiwa_katika_shambulio_la_iran_wasema_jeshi_limewatelekeza
Wanajeshi kadhaa wa Marekani waliojeruhiwa katika moja ya mashambulizi makali ya ndege zisizo na rubani yaliyofanywa na Iran nchini Kuwait wamesema mfumo wa matibabu wa jeshi umewatelekeza na kuwaacha bila ya kuwapatia matibabu ya kutosha.
(last modified 2026-10-08T07:23:11+00:00 )
Oct 08, 2026 03:15 UTC
  • Askari wa US waliojeruhiwa katika shambulio la Iran wasema jeshi limewatelekeza

Wanajeshi kadhaa wa Marekani waliojeruhiwa katika moja ya mashambulizi makali ya ndege zisizo na rubani yaliyofanywa na Iran nchini Kuwait wamesema mfumo wa matibabu wa jeshi umewatelekeza na kuwaacha bila ya kuwapatia matibabu ya kutosha.

Wanajeshi hao wamesema, walilazimika kutafuta matibabu wenyewe baada ya shambulio dhidi ya kituo cha operesheni za kivita cha Marekani katika Bandari ya Shuaiba nchini Kuwait mnamo tarehe mosi Machi.

Askari sita wa Kikosi cha Akiba cha Jeshi la Marekani waliuawa na wengine zaidi ya 30 walijeruhiwa wakati shambulio hilo la kulipiza kisasi la Iran lilipopiga kituo hicho.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, wanajeshi tisa waliojeruhiwa wamesema, walikumbana na mapungufu makubwa katika kupatiwa huduma za matibabu kufuatia shambulio hilo; ambapo baadhi yao wameeleza kuwa, waliachwa wajitibu wenyewe au kusubiri kwa wiki na miezi kadhaa ili kupata matibabu maalumu.

Luteni Kanali wa Jeshi, Arturo Lincón, amesema vipande vya chuma vilimpiga kwenye taya na shingo, vikakata mshipa wa damu na kuganda kwenye mfupa wa uti wa mgongo. Licha ya kugunduliwa kuwa na jeraha la kiwewe la ubongo na kuwa katika hatari ya kupata kiharusi, amesema jeshi halikuona hali yake kuwa mbaya kiasi cha kuhitaji kulazwa katika Kituo cha Matibabu cha Kanda cha Landstuhl nchini Ujerumani, kwa sababu hakuwa amekamilisha taratibu za kusajiliwa kama "majeruhi wa vitani".

"Nilikuwa peke yangu tu, au angalau ndivyo nilivyohisi," ameeleza Lincón.
Amesema alikaa siku kadhaa bila dawa za maumivu, na baadaye akatumia wiki saba akipata matibabu maalumu ya nje (bila kulazwa) katika Kituo cha Kitaifa cha Matibabu ya Kijeshi cha Walter Reed. Vipande vya chuma vingali vimeganda mgongoni mwake kwa sababu madaktari waliona kuviondoa ni hatari sana kutokana na kukaribia uti wa mgongo.

Meja Stephen Ramsbottom yeye amesema, alisubiri kwa zaidi ya miezi minne kupata matokeo ya kipimo cha MRI baada ya vipande vya chuma kuondolewa kichwani mwake.

"Imenibidi nijishughulikie mwenyewe kwa kila kitu," ameeleza Ramsbottom na kuongezea kwa kusema: "Inakatisha tamaa sana."

Meja Billy Key, ambaye alipata jeraha la kichwa, kupoteza uwezo wa kusikia na uharibifu wa mapafu kutokana na kuvuta moshi, amesema, hakupata matibabu maalumu hadi katikati ya mwezi wa Aprili. "Ilichukua muda mrefu sana," amefichua askari huyo wa jeshi la Marekani…/