Marekani yaiingia tena mwilini Afrika Kusini
-
Marekani yaiingia tena mwilini Afrika Kusini
Marekani imeanzisha mzozo mpya na Afrika Kusini na kupelekea kuzuka majibizano makali ya hadharani kati ya Waziri wa Afrika Kusini wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano, Ronald Lamola, na Balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini, Brent Bozell.
Waziri huyo wa Afrika Kusini amelazimika kujibu vitendo na kauli za huko nyuma za balozi wa Marekani na kusema kuwa balozi huyo anapaswa "kuondoka jikoni" kama amechoshwa na mazungumzo na hana imani tena na ushirikiano wa kidiplomasia na Pretoria.
Akijifanya mtu aliyedhulumiwa licha ya kwamba yeye ndiye aliyeanzisha ugomvi, balozi wa Marekani ameandika kwenye mtandao ya kijamii kwamba: "Haya tena. Tusi jingine hilo binafsi kutoka kwa Waziri Lamola dhidi ya kiongozi wa Marekani (safari hii ni dhidi yangu mimi)."
Kauli za Waziri Lamola alizozitoa baada ya kushindwa kuvumilia ubeberu wa Marekani, zilichapishwa na gazeti la "Sunday Times" la Afrika Kusini siku ya Jumapili, ikiwa ni siku chache baada ya Afrika Kusini kuwasilisha malalamiko rasmi ya dhdi ya balozi wa Marekani nchini humo ambaye anafanya uchochezi na vitendo visivyo vya kidiplomasia.
Waziri Lamola alisema ameshangazwa na kauli za Bozell zilizodokeza kuwa Washington imechoshwa na mazungumzo ya mara kwa mara na Pretoria.
Waziri Lamola pia amesema: "Huwezi kuwa na mwanadiplomasia anayesema muda wa mazungumzo umekwisha. Kazi yetu ni kuzungumza."
Pia alimlaumu vikali balozi huyo wa Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya Afrika Kusini tena kwa kauli na vitendo vya hadharani.
Tarehe 29 Septemba 2026, Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini ilimwita Bozell kwenda kutoa maelezo kuhusu tabia zake zisizo za kidiplomasia. Hayo yalikuwa ni malalamiko rasmi ya tatu yaliyowasilishwa kwa balozi huyo wa Marekani tangu alipowasili Pretoria mwezi Februari kutokana na uchochezi wake na kuingilia masuala yasiyomuhusu.
Popote pale dola la kibeberu la Marekani linapotia mguu wake huwa hapabaki salama. Viongozi wa juu hadi wa chini wa Marekani ni maarufu kwa kutoheshimu sheria za kimataifa wala haki za kujitawala mataifa ya dunia na kujiamulia mambo yao kwa uhuru.