Ghana yatangaza azma ya kujiunga na kundi la kiuchumi la BRICS
Ghana imesema itawasilisha rasmi ombi la kujiunga na kundi la kiuchumi la BRICS baada ya Baraza la Mawaziri la Rais John Dramani Mahama kuidhinisha hatua hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, amesema uamuzi huo ni sehemu ya juhudi za Ghana kupanua ushirikiano wake wa kimataifa na kutengeneza fursa zaidi za maendeleo ya kiuchumi.
Ablakwa amebainisha kuwa, hatua hiyo ni miongoni mwa mambo makuu yaliyoamuliwa na serikali ya Rais Mahama.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la News Agency, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana amesema: “Jambo jingine kubwa ambalo nalifichua kwa mara ya kwanza kwa wananchi wa Ghana ni kwamba Baraza la Mawaziri la Rais John Dramani Mahama limeamua kuwa Ghana inapaswa kuwasilisha rasmi ombi la kujiunga na BRICS.”
Waziri huyo amesisitiza kuwa kujiunga na BRICS hakumaanishi kwamba Ghana itasitisha uhusiano wake na washirika wake wa jadi. Badala yake, uanachama huo unakusudiwa kuongeza chaguo na fursa za ushirikiano wa maendeleo.
Ablakwa amekumbusha kuwa Ghana tayari ni mwanachama wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, pamoja na kuwa mwanachama mwanzilishi wa taasisi za kifedha za kimataifa za Afrika.
“BRICS inatupa fursa ya kuwa na chaguo katika maendeleo, na ni muhimu kuwa na chaguo,” ameongeza waziri huyo.
Ablakwa amesema hatua hiyo iliafikiana na lengo la serikali ya Mahama la kuiondoa Ghana katika hali ya udumavu wa kiuchumi na kuielekeza
kwenye ukuaji wenye kuleta mabadiliko ya muda mrefu.
Amezitaja India, Brazil na China kuwa ni washirika muhimu wa kiuchumi wa Ghana, akisisitiza pia kuongezeka kwa biashara kati ya Ghana na India. Kwa mujibu wa waziri huyo, biashara ya nchi hizo mbili imeongezeka zaidi ya mara mbili, kutoka takribani dola bilioni 3 mwaka 2024 hadi karibu dola bilioni 7.
Ablakwa amesema, serikali ya Ghana inajiandaa kuwasilisha ombi rasmi la kuwa mwanachama na itatafuta uungwaji mkono kutoka kwa wanachama wa BRICS.
Ameongeza kuwa Ghana tayari imeomba rasmi msaada wa India katika jitihada zake za kujiunga na BRICS na imepokea majibu yenye kutia moyo kutoka kwa Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India,
ambaye alikuwa katika ziara rasmi jijini Accra…/