Baada ya miaka mitatu, hatimaye Israel yakiri imeshindwa kuidhibiti HAMAS
-
Baada ya miaka mitatu, hatimaye Israel yakiri imeshindwa kuidhibiti HAMAS
Miaka mitatu tangu utawala katili wa Kizayuni ulipoanzisha vita vya kinyama dhidi ya wananchi wa Ghaza, na baada ya kupita miaka miwili na nusu tangu Netanyahu adai amepata ushindi huko Ghaza, hivi sasa vyombo vya usalama vya Israel vinakiri kuwa vimeshindwa kuimaliza na kuidhibiti Hamas na bado harakati hiyo ina silaha na nguvu zake na ndiyo inayodhibiti ukanda huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, hali halisi ilivyo kwenye medani ya vita ni ngumu zaidi kuliko walivyokuwa wanajidanganya Wazayuni na serikali yao ya kibeberu. HAMAS bado ina nguvu na si rahisi kuimaliza harakati ambayo imekita mizizi ndani ya damu za wananchi.
Vyombo vya usalama vya Israel sasa vimelazimika kukiri hadharani kwamba madai ya ushindi yaliyotangazwa na Netanyahu ni uongo mtupu kwani Hamas bado iko imara, bado imehifadhi silaha zake na wanajeshi wa Israel mpaka hivi sasa wameemewa na hawajui watamaliza vipi vita vya Ghaza kwani hawawezi kudai kuwa wameshinda na ni vigumu mno kwao kukubali kushindwa na kundi dogo tu la wanamapambano wa Kiislamu.
Elisha Ben Kimon, mwandishi wa habari za kijeshi wa gazeti la "Yedioth Ahronoth" ameripoti kuwa, maafisa ndani ya vyombo vya usalama vya Israel wanakiri kwamba miaka mitatu baada ya "Janga la Oktoba 7" na miaka miwili na nusu baada ya Benjamin Netanyahu kudai kuwa Israel imeshinda vita, hali huko Ghaza bado iko mbali sana na kutangaza kushinda vita. Ukweli wa wazi ni kwamba Hamas ndiyo inayoendelea kutawala Ukanda wa Ghaza.
Ben Kimon aidha ameandika kuwa, vyombo vya usalama vya Israel kwa sasa vinafanya tathmini ya vita hivyo vya miaka mitatu na kuchora picha ya matukio ya Ghaza vikikiri kuwa hali bado ni ngumu sana kwa Wazayuni.
"Jambo muhimu na la msingi ni kwamba Hamas kwa hakika bado ipo imara na haijapokonywa silaha zake. Tab'an sababu kuu ya jambo hilo ni kukosekana mpango wa kisiasa uliopangwa vizuri kwa ajili ya mustakabali wa ukanda huo," amesema mwandishi huyo wa gazeti la Kizayuni.