Iran yalaani misimamo ya nyuso mbili ya Ufaransa kuhusu maandamano
-
Esmaeil Baghaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametilia mkazo umuhimu na wajibu wa viongozi wa Ufaransa kuheshimu haki za binadamu na kuacha ukandamizaji wa kikatili dhidi ya maandamano ya amani nchini humo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei, ameandika ujumbe kwenye mtandao wa X akizungumzia hatua za kikatili zinachochukuliwa na askari usalama wa Ufaransa dhidi ya maandamano ya amani ya wanafunzi na kuilaumu nchi hiyo ya Ulaya kwa kutoheshimu haki za binadamu na kuwa na nyuso mbili katika misimamo yao.
Mwezi Januari 2026, na katika kutoa maoni yake kuhusu Iran, Ufaransa ilizungumzia umuhimu wa kuheshimiwa kile ilichodai ni "mkusanyiko wa amani" na kuitaka serikali ya Iran kuonesha ustahimilivu mbele ya waandamanaji.
Ingawa viongozi wa Ufaransa walikuwa wanajua vyema kwamba kilichotokea Iran hayakuwa maandamano ya amani bali lilikuwa ni jaribio la mapinduzi lililofanyika kwa mauaji makubwa ya kigaidi ya magenge yanayofadhiliwa na hayo hayo madola ya kibeberu, lakini viongozi wa Ufaransa walijitokeza hadharani na bila ya aibu kuwaunga mkono magaidi waliokuwa wanafanya ukatili dhidi ya wananchi na maafisa wa Iran.
Hivi sasa kuna maandamano makubwa ya amani yanaendelea huko Ufaransa lakini madola yote ya Magharibi na hasa viongozi wa Ufaransa wanayaita maandamano hayo ya wanafunzi nchini humo kuwa ni "vurugu za mijini."
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa sasa amesahau kutumia neno ustahamilifu na anaendelea kuchochea hatua kali dhidi ya wanafunzi wanaopigania haki zao kutoka na mfumo mbovu wa kielimu wa nchi hiyo ya Ulaya. Moja ya sababu za maandamano ya wanafunzi ya hivi sasa huko Ufaransa ni kulalamikia uchache wa walimu, ubovu wa vitendea kazi, kurundikwa wanafunzi wengi darasa moja na matatizo mengine chungu nzima ya mfumo wa kielimu wa dola hilo la kikoloni.
Ni wazi kuwa vurugu dhidi ya polisi, uchomaji moto, na uharibifu wa mali ya umma si mambo yanayoweza kuhalalishwa, na kila serikali lazima itachukuka hatua kuzuia vitendo hivyo, lakini tatizo linakuja pale viongozi wa Ufaransa na madola mengine ya kibeberu yanapojiweka mstari wa mbele kulaumu wengine kwa vitendo hivyo hivyo ambavyo zenyewe tawala hizo za kibeberu zinavitenda kukabiliana na waandamanaji.