Imarati na Israel zapapurana, safari za ndege zapigwa marufuku
Shirika la usalama wa ndani la Israel limepinga uendeshaji wa safari za ndege kutoka Dubai kwenda Tel Aviv zilizokusudiwa kuwarejesha abiria wa utawala wa Kizayuni waliokwamba Dubai.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kuongezeka mapapurano na mivutano baina ya viongozi wa utawala wa Kizayuni na wa Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) hasa katika suala zima la kusimamia usalama wa viwanja vya ndege.
Shirika la Habari la Mehr limeinukuu televisheni ya i24NEWS ikitangaza kuwa, shirika la usalama wa ndani la utawala wa Kizayuni lijulikanalo kwa jina la Shin Bet (Shabak) limetangaza kusimamishwa safari za ndege za mashirika ya Muungano wa Falme za Kiarabu zilizopangwa kuwarejesha abiria wa Israel waliokwama Dubai.
Ripoti hiyo inaonesha kuweko mzozo mkubwa kati ya Shin Bet na maafisa wa Imarati kuhusu taratibu za ukaguzi wa usalama katika Uwanja wa Ndege wa Dubai huku utawala wa Kizayuni ukionesha wazi kwamba hauna imani na maafisa usalama wa Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati).
Kuongezeka mvutano huo kumekuja baada ya "tukio la FlyDubai" lililogubikwa na utata mwingi na riwaya zinazogongana na zisizo na mantiki ambazo zinazuia kujulikana nini hasa kilitokea ndani ya chumba cha marubani na ndani ya ndege ya FlyDubai iliyokuwa inaelekea Tel Aviv.
Kuna maelezo mengi yanayokinzana kuhusu jaribio linalodaiwa kufanywa na rubani mwenza anayedaiwa kuwa ni raia wa Oman la kutaka kuangusha ndege iliyokuwa imebeba abiria 150 wa Israel.
Kufuatia tukio hilo, shirika la ndege la FlyDubai lilitangaza kusimamisha safari zake kwenda katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel. Shirika hilo la Muungano wa Falme za Kiarabu lilitangaza kusimamisha safari hizo kwa muda wa siku sita.
Mashirika ya ndege ya utawala wa Kizayuni wa Israel nayo yalikuwa yamepanga kuwarejesha Wazayuni waliokwama huko Dubai lakini yamekumbana na vikwazo mbalimbali hasa vya maafisa usalama wa utawala wa Kizayuni ambao hawana imani na maafisa usalama wa Imarati.