Iran: Makombora yetu mapya yana kasi zaidi na yanapiga mbali zaidi
Msemaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia upeo na kasi ya makombora mapya ya Iran na kusisitiza kuwa, makombora yetu mapya yanapiga umbali mkubwa zaidi na kwa kasi kubwa zaidi.
Brigedia Jenerali Mohammad Akrami-Nia amezungumza na waandishi wa habari na kusema: "Sababu ya kuchukulia hatua hii ni kwamba adui sasa yuko mbali zaidi na pwani zetu, yuko kwenye umbali wa hadi kilomita 1,000 ndio maana tumeamua kuboresha makombora haya kuendana na hali ilivyo."
Msemaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia pia tajiriba iliyopata Iran kwenye Vita vya Ramadhani vilivyoanzshwa na Marekani na utawala wa Kizayuni tarehe 28 Februari 2026 dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema: "Wakati wa vita hivyo, tulifikia uamuzi kuwa ni lazima kabisa tuongeze kasi na upeo wa makombora yetu..."
Amesema: "Hatua kubwa zimepigwa kuhusiana na kasi ya makombora na uwezo wa kulenga shabaha kwa usahihi wa hali ya juu; vizazi vipya vya makombora yetu vina uwezo mkubwa zaidi."
Akizungumzia utendaji wa makombora yaliyotumika wakati wa Vita vya Ramadhani, msemaji wa Jeshi la Iran amesema: "Makombora tuliyotumia wakati wa mgogoro huo, hasa makombora ya Kikosi cha Nchi Kavu ambayo yalitumika kushambulia kambi za adui nchini Kuwait na makombora ya Jeshi la Majini aina ya 'cruise' yaliyopiga meli za adui, yalifanya kazi vizuri sana na yalikuwa na ufanisi mkubwa."
Brigedia Jenerali Akrami-Nia ameendelea kusema: "Pamoja na mafanikio yote hayo, lakini tulifikia uamuzi kuwa ni lazima tuongeze kasi na upeo wa makombora haya, kwa kuwa adui sasa yuko mbali zaidi na pwani zetu, umbali wa hadi kilomita 1,000."
Akijibu swali iwapo uboreshaji huou unahusu makombora yote ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Brigedia Jenerali Mohammad Akrami-Nia amesema: "Ndiyo, hili linahusu makombora yetu yote."