Iran: Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa hayapaswi kuweko Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141938-iran_makao_makuu_ya_umoja_wa_mataifa_hayapaswi_kuweko_marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa: Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa hayapaswi kuweko nchini Marekani kwani nchi hiyo si mwenyeji mzuri hata kidogo wa chombo hicho kikubwa zaidi cha kimataifa duniani.
(last modified 2026-10-04T11:08:28+00:00 )
Oct 04, 2026 11:07 UTC
  • Iran: Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa hayapaswi kuweko Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa: Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa hayapaswi kuweko nchini Marekani kwani nchi hiyo si mwenyeji mzuri hata kidogo wa chombo hicho kikubwa zaidi cha kimataifa duniani.

Esmaeil Baghaei amesema hayo leo mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kwamba: "Ujumbe wa Iran ukiongozwa na Rais (Pezeshkian) ulishiriki ukiwa na watu wachache kutokana na vikwazo vingi vya visa vilivyowekwa na Marekani, lakini ujumbe huo wa watu wachache wa Iran ilikuwa na tija kubwa. Ilikuwa muhimu kwetu kutumia fursa ile kwenda kuutangazia ulimwengu uhalisia wa dhulma inazofanyiwa Iran, na tulishuhudia moja ya ushiriki wenye mafanikio makubwa zaidi wa Iran katika majukwaa ya kimataifa."

"Mikutano iliyofanyika New York ilikuwa na manufaa makubwa na yenye ufanisi katika kufafanua misimamo ya Iran na kuonesha mantiki iliyojikita sawasawa ya misimamo na hatua zake."

Akizungumzia ziara ya waziri mkuu wa utawala wa wa Kizayuni nchini Imarati (UAE), Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Ushauri wetu kwa nchi zote jirani ni kuzingatia haki za ujirani mwema na kutoruhusu rasilimali na ardhi zao kutumiwa vibaya na watu baki."

"Tumeeleza waziwazi malalamiko yetu kwa nchi jirani. Haya ni matakwa tunayoyasisitizia kila tunapopata fursa. Pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mazungumzo yalifanyika na maafisa kutoka karibu nchi zote za Ghuba ya Uajemi."

Amma kuhusu Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kuweko Marekani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, "Marekani haina ustahiki wa kuwa mwenyeji wa Umoja wa Mataifa... Marekani si mwenyeji anayefaa kwa Umoja wa Mataifa."

Amesema: "Inaonekana kwamba baada ya kushindwa kuzuia ujumbe wa Iran kushiriki vikao vya Umoja wa Mataifa na baada ya kushindwa kufanikisha mpango wao wa kuionesha Iran kuwa ni nchi iliyotengwa, viongozi wa Marekani waliamua kutumia hadithi za kubuni ambazo hazina hata hadhi ya kujibiwa."