Iran yaangamiza mitandao minne ya kijasusi yenye uhusiano na Marekani na Israel
-
Iran yaangamiza mitandao minne ya hujuma yenye uhusiano na Marekani na Israel
Wizara ya Kiintelijensia ya Iran imetangaza kuwa, imevunjilia mbali mitandao minne ya hujuma inayoungwa mkono na Marekani na utawala haramu Israel katika mji wa Sirjan, mkoani Kerman, kusini mwa Iran.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, watu 31 wametiwa mbaroni wakituhumiwa kuwa sehemu ya mitandao hiyo, ambayo ilituhumiwa kupanga kuchochea machafuko na kufanya vitendo vya hujuma.
Wizara ya Usalamay a Iran imesema operesheni hiyo ilifanikishwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi pamoja na ufuatiliaji wa kiintelijensia.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mitandao hiyo ilikuwa ikitumia majina yaliyovutia vijana na kuwapa majukumu maalumu ya kushiriki katika wito wa maandamano na machafuko nchini. Aidha, mamlaka zinasema zilikuta idadi kubwa ya chupa za Molotov ambazo hutumika kama silaha za moto zilizotengenezwa kienyeji” na vifaa vilivyokusudiwa kuharibu kamera za ulinzi mijini.
Wizara hiyo pia imeeleza kuwa baadhi ya wanachama wa mitandao hiyo walihusika katika vitendo vya vurugu na uharibifu vilivyotokea wakati wa machafuko ya Januari, ikiwemo kuchomwa moto kwa jengo la serikali, kuharibiwa benki na majengo ya umma, pamoja na kushambuliwa kituo cha polisi katika jaribio la kutwaa silaha.
Maandamano ya amani yalianza katika maeneo mbalimbali ya Iran mwishoni mwa Desemba 2025, yakichochewa zaidi na malalamiko ya kiuchumi, yakiwemo kushuka kwa thamani ya sarafu ya rial na kupanda kwa gharama za maisha. Maandamano hayo yalianza hasa miongoni mwa wafanyabiashara wa Soko Kuu la Tehran (Bazaar) na baadayye kuenea katika maeneo mengine ya nchi.
Baada ya serikali kuingilia kati na Rais Masoud Pezeshkian kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na wawakilishi wa vyama na jumuiya za wafanyabiashara, hali ilionekana kutulia kwa muda. Hata hivyo, maandamano yaliongezeka tena kuanzia Januari 8, 2026, wakati mawasiliano ya intaneti na simu yalipowekewa vikwazo.