Wanademokrati wakosoa kuendelezwa vita vya Trump dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141912-wanademokrati_wakosoa_kuendelezwa_vita_vya_trump_dhidi_ya_iran
Viongozi wa chama cha Democratic nchini Marekani wameendelea kuikosoa serikali ya Rais Donald Trump kuhusu vita vya Marekani dhidi ya Iran, wakitaka vita hivyo vikomeshwe na mamlaka ya Congress yaheshimiwe. Kiongozi wa Democrats katika Seneti, Chuck Schumer amesema chama chake hakitaki kuunga mkono kuendelezwa kwa vita ambavyo, kwa maelezo yake, havijaidhinishwa na Congress na havina mpango wa wazi wa kumalizika.
(last modified 2026-10-03T11:26:47+00:00 )
Oct 03, 2026 11:25 UTC
  • Wanademokrati wakosoa kuendelezwa vita vya Trump dhidi ya Iran
    Wanademokrati wakosoa kuendelezwa vita vya Trump dhidi ya Iran

Viongozi wa chama cha Democratic nchini Marekani wameendelea kuikosoa serikali ya Rais Donald Trump kuhusu vita vya Marekani dhidi ya Iran, wakitaka vita hivyo vikomeshwe na mamlaka ya Congress yaheshimiwe. Kiongozi wa Democrats katika Seneti, Chuck Schumer amesema chama chake hakitaki kuunga mkono kuendelezwa kwa vita ambavyo, kwa maelezo yake, havijaidhinishwa na Congress na havina mpango wa wazi wa kumalizika.

Schumer pia amekosoa vitisho vya Trump dhidi ya Iran, akisema vitisho hivyo vinaongeza hatari ya mzozo huo kuendelea. Ikumbukwe kuwa, katika hotuba yake ya Seneti Septemba 22, 2026, Schumer alimtaka Trump kukomesha vita na kurejea kwenye njia ya diplomasia.

Wabunge kadhaa wa Democrats pia wamekuwa wakisukuma azimio la War Powers Resolution, linalolenga takwa la kusitishwa kwa operesheni za kijeshi za Marekani nchini Iran.

Wakosoaji wa Democrats pia wameelekeza ukosoaji wao kwenye gharama za vita, vifo vya wanajeshi wa Marekani na athari za mzozo huo kwa bei ya mafuta na hali ya usalama katika Mashariki ya Kati. Hata hivyo, ndani ya chama cha Democrats kuna mitazamo tofauti kuhusu sera ya Marekani mkabala na Iran na namna ya kukabiliana na mpango wake wa nyuklia.

Kwa upande mwingine, Seneta Elizabeth Warren wa chama cha Democratic kutoka jimbo la Massachusetts amesema, vita vya Marekani dhidi ya Iran vinaongeza gharama kwa familia za Marekani, ikiwemo gharama za nyumba. Warren ameeleza kuwa, kupanda kwa bei za nishati na viwango vya riba kunaongeza gharama za mikopo ya nyumba. Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha pia kuwa mzozo huo umehusishwa na kupanda kwa gharama za nishati na viwango vya mikopo ya nyumba nchini Marekani.

Naye Hakeem Jeffries, kiongozi wa Wademokrat katika Baraza la Wawakilishi kutoka New York, amekosoa hali ya uchumi nchini Marekani, akitaja kupanda kwa mfumuko wa bei na kupungua kwa ongezeko la ajira. Amesema vita dhidi ya Iran vimekuwa na athari kubwa kwa uchumi na kwamba Wademokrat wataendelea kushinikiza sera zinazolenga kupunguza gharama za maisha.