Putin: Dunia inastaajabishwa na ushujaa na ustahimilivu wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141880-putin_dunia_inastaajabishwa_na_ushujaa_na_ustahimilivu_wa_iran
Rais Vladimir Putin wa Russia alisema jana Alkhamisi kuwa watu kote duniani wanastaajabishwa na ushujaa wa taifa la Iran.
(last modified 2026-10-02T02:59:02+00:00 )
Oct 02, 2026 02:58 UTC
  • Putin: Dunia inastaajabishwa na ushujaa na ustahimilivu wa Iran

Rais Vladimir Putin wa Russia alisema jana Alkhamisi kuwa watu kote duniani wanastaajabishwa na ushujaa wa taifa la Iran.

Shirika la Habari la Fars (Kitengo cha Kimataifa) – limeripoti habari hiyo na kumnukuu Rais Putin akisema hayo wakati alipokuwa anazungumza katika mkutano wa 23 wa kila mwaka wa "Klabu ya Majadiliano ya Valdai," na kusifu mwenendo wa taifa la Iran na kuelezea mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Ali Larijani, kama "kosa kubwa."

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, Rais wa Russia ameusifu uongozi wa Iran kwa kuwa na rasilimali watu yenye uwezo na ujuzi wa hali ya juu akisema: "Dunia nzima inafuatilia kwa karibu matukio ya hivi sasa na inastaajabishwa na ujasiri na ushujaa wa taifa la Iran pamoja na ustahimilivu wake."

Putin pia amesema: "Tunatumai kuwa Lango-Bahari la Hormuz litafunguliwa na vikwazo dhidi ya Iran vitaondolewa kama ambavyo tunaamin kwamba ni haki ya Iran kudai hivyo."

Kuhusu mauaji ya Dk Ali Larijani, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran, Rais wa Russia amesema: "Mauaji ya Ali Larijani yalikuwa kosa kubwa. Nilimfahamu binafsi. Alikuwa mtu mwenye mtazamo chanya, tayari kujadili masuluhisho ambayo yangelilinufaisha taifa la Iran."

Tarehe 17 Machi 2026, katikati ya uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran na ikiwa ni sehemu ya kampeni ya mauaji yaliyokuwa yanafanywa na viongozi magaidi wa Marekani na Israel dhidi ya maafisa wa ngazi za juu wa kisiasa na kijeshi wa Iran, utawala wa kigaidi wa Israel ulimshambulia kwa makusudi Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Dk Ali Larijani na kumuua shahidi kidhulma.

Mbali na Dk. Ali Larijani, mwanawe Morteza Larijani, naibu wake Alireza Bayat na baadhi ya walinzi wao nao pia waliuawa shahidi kwenye ukatili huo. Jinai hiyo ilizua hisia hasi kutoka kwa nchi mbalimbali duniani dhidi ya Israel. Viongozi wa Russia nao pia walilaani mauaji hayo ya kikatili.