Atwan achambua uongo wa Wazayuni kuhusu FlyDubai, atoa sababu 11
Abdel Bari Atwan mmoja wa wachambuzi mahiri na waandamizi wa masuala ya Ulimengu wa Kiislamu na Kiarabu ametoa sababu 11 zinazofichua uongo na ukidhabi wa Wazayuni katika riwaya yao kuhusu tukio la FlyDubai iliyokuwa inaelekea Israel.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Abdel Bari Atwan, ameandika makala kwenye tovuti ya *Rai al-Youm* na kusema kwamba ushahidi wote unaonesha kuwa tukio hilo lililohusisha ndege ya Imarati ya "FlyDubai" iliyokuwa ikielekea Tel Aviv lilikuwa ni tukio lililopangwa na kuratibiwa kwa ustadi wa hali ya juu na na mashirika ya kijasusi ya utawala wa Kizayuni.
Akibainisha kuwa nia halisi nyuma ya tukio hili bado haijajulikan wazi, amesma kuwa simulizi ya Israel kuhusu tukio hilo imejaa uongo unaojigonga wenyewe na wenye mantiki dhaifu. Kubwa zaidi kati ya hizo ni madai ya kutokea ugomvi wa maneno ndani ya chumba cha marubani kati ya rubani mkuu na rubani msaidizi, ikifuatiwa na rubani msaidizi kudaiwa kumchoma kisu rubani mkuu na kusababisha damu kumtoka katika jaribio la kuangusha ndege hiyo na kuua watu wote 174 waliokuwemo. Simulizi hiyo inadai zaidi kuwa uingiliaji kati wa abiria ulizima njama.
Atwan aliwasilisha sababu 11 zinazoashiria kuwa shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni ndilo lililokuwa nyuma ya tukio hilo. Hapa tutataja baadhi:
Kwanza: Awali, ilielezwa kuwa rubani mkuu alikuwa mwenye asili ya Russia na rubani msaidizi aliyeshambulia alikuwa raia wa Ukraine. Simulizi hiyo baadaye ilibadilishwa na kudai kuwa rubani mkuu alikuwa raia wa Imarati na rubani msaidizi alikuwa raia wa Oman. Baadaye, maelezo hayo yalirekebishwa na kusema kuwa rubani mkuu alikuwa raia wa India na rubani msaidizi alikuwa raia wa Oman.
Pili: Hadi sasa, hatujasikia taarifa rasmi au maoni yoyote kutoka Saudi Arabia — nchi ambayo inasemekana ndege hiyo ilitua kwa dharura.
Tatu: Kwa nini ndege hiyo ilijiondoa katika anga la Jordan na kuamua kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tabuk nchini Saudi Arabia? Uwanja wa Ndege wa Tabuk hauko mbali na Uwanja wa Ndege wa Eilat huko Israel au Uwanja wa Ndege wa Sharm El-Sheikh nchini Misri na Uwanja wa Ndege wa Aqaba pia uko karibu sana.
Nne: Je, ilikuwa ni bahati mbaya kuweko marubani wawili wa Israel waliobobea katika aina hii ya ndege, na timu ya madaktari kati ya abiria?
Tano: Chumba cha marubani hakiwezi kufunguliwa kutokea nje; hata hivyo, simulizi dhaifu na isiyo na msingi ya utawala wa Kizayuni inadai kuwa rubani aliyejeruhiwa alisimama na kufungua mlango kwa ajili ya abiria waliokuwa wakivamia chumba hicho. Je, rubani msaidizi mwenye nguvu zaidi kimwili na ambaye hakujeruhiwa alikuweko wapi wakati huo na kwa nini hakumzuia?
Sita: Simulizi ya Kizayuni ilimtaja rubani wa Kihindi kama "Smith Mashar," lakini hadi sasa, hawajafichua jina la rubani msaidizi "wa Kiomani" anayetuhumiwa kujaribu kuharibu ndege hiyo.
Saba: Miri Regev, Waziri wa Uchukuzi wa utawala wa Kizayuni, alionesha kushangazwa na kuwepo rubani msaidizi wa Kiomani katika chumba cha marubani, akibainisha kuwa makubaliano kati ya Israel na Imarati yanazuia shirika la Flydubai kuajiri marubani au marubani wasaidizi kutoka mataifa ambayo hayana uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni; hii inaashiria kuwa rubani huyo msaidizi hakuwa raia wa Oman.
Nane: Siku mbili kabla, Netanyahu alikuwa ameonya kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulizi wakati huu unapokaribia uchaguzi wa utawala wa Kizayuni; hii inaonyesha kuwa alikuwa na taarifa kuhusu njama hiyo na labda hata alikuwa na uhakika kwamba ingefanikiwa kuharibu ndege hiyo na hivyo kupata kisingizio cha uwezekano wa kufanya uchokozi mya dhidi ya Iran.
Tisa: Israel Katz, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni, alisisitiza kuwa ndege hiyo ilikuwa imelengwa na shambulio la kigaidi; hata hivyo, silaha, risasi na mada za milipuko vilivyotumika katika operesheni hiyo, viko wapi?
Kumi: Je, abiria wa Israel — aliyeitwa mwokozi — na wenzake walifanikiwaje kuingia katika chumba cha marubani, kufungua mlango, kuchukua udhibiti wa ndege, na kumdhibiti rubani msaidizi wakati ndege hiyo ilipokuwa ikishuka kwa kasi kubwa mno, ya futi 15,000 kwa sekunde?
Kumi na moja: Abiria aliyedai kuokoa ndege hiyo alikiri kuwa yeye si rubani na alijifunza kurusha ndege kwa kutazama video tu! Hicho si kioja cha mwaka?
Mwandishi huyo amegusia historia ya utawala wa Kizayuni ya kubuni simulizi za uongo na chapwa kama hizo hasa kuhusiana na operesheni ya tarehe 7 Oktoba na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wa Palestina na kusisitiza kuwa Wazayuni hawatasita kupanga shambulio la "kigaidi" dhidi ya ndege ya Imarati, wakilitumia kama kisingizio cha kutenda uhalifu na jinai kubwa zaidi za kivita.