China yataka marekebisho ya mfumo wa kimataifa wa Haki za Binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141876-china_yataka_marekebisho_ya_mfumo_wa_kimataifa_wa_haki_za_binadamu
China, kwa niaba ya nchi 71, imetaka kufanyiwa marekebisho mfumo wa kimataifa unaosimamia haki za binadamu, kwa kuongozwa na Mpango wa Utawala wa Kimataifa (Global Governance Initiative).
(last modified 2026-10-02T02:54:51+00:00 )
Oct 02, 2026 02:53 UTC
  • China yataka marekebisho ya mfumo wa kimataifa wa Haki za Binadamu

China, kwa niaba ya nchi 71, imetaka kufanyiwa marekebisho mfumo wa kimataifa unaosimamia haki za binadamu, kwa kuongozwa na Mpango wa Utawala wa Kimataifa (Global Governance Initiative).

Jia Guide, Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva na mashirika mengine ya kimataifa yaliyoko Uswisi, ametoa wito huo katika kikao cha 63 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, akizungumza kwa niaba ya nchi hizo 71.

Ametaka kuwepo mfumo wa kimataifa wa haki za binadamu ulio wa haki, wenye mantiki na unaojumuisha nchi zote, chini ya mwongozo wa Mpango wa Utawala wa Kimataifa.

Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amebainisha kuwa, kutokana na hali ya sasa ya dunia kuwa tata na isiyotabirika, mfumo wa kimataifa unaosimamia haki za binadamu unahitaji marekebisho makubwa. Kwa msingi huo, China imewasilisha mapendekezo manne yafuatayo: Mosi, kuweka wananchi katika kitovu cha haki za binadamu.

Pili, kuheshimu usawa wa mamlaka ya nchi zote.

Tatu, kuzingatia haki na kupinga matumizi ya kisiasa ya haki za binadamu.

Na nne, kuheshimu sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa

China imesisitiza umuhimu wa kuzingatia utawala wa sheria za kimataifa na kulinda malengo pamoja na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mapendekezo hayo yameandaliwa na kuwasilishwa kwa niaba ya Kundi la Marafiki wa Utawala wa Kimataifa (Group of Friends of Global Governance), lenye makao yake mjini Geneva.

Hatua hiyo imekuja zaidi ya mwaka mmoja baada ya Rais wa China, Xi Jinping, kuwasilisha Mpango wa Utawala wa Kimataifa.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa Iran ni miongoni mwa wanachama wa Kundi la Marafiki wa Utawala wa Kimataifa.