Waziri wa Ulinzi wa Pakistan: Dunia haiamini tena propaganda za Waisraeli
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141898-waziri_wa_ulinzi_wa_pakistan_dunia_haiamini_tena_propaganda_za_waisraeli
Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, akijibu hatua ya Waziri Mkuu wa utawala wa Israel ya kutumia tukio la ndege ya Flydubai kwa madhumuni ya propaganda, amesema kuwa maoni ya umma duniani yamegeuka na kuwa dhidi ya Benjamin Netanyahu, na kwamba watu hawaamini tena propaganda za Waisraeli.
(last modified 2026-10-03T02:55:03+00:00 )
Oct 03, 2026 02:53 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Pakistan: Dunia haiamini tena propaganda za Waisraeli

Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, akijibu hatua ya Waziri Mkuu wa utawala wa Israel ya kutumia tukio la ndege ya Flydubai kwa madhumuni ya propaganda, amesema kuwa maoni ya umma duniani yamegeuka na kuwa dhidi ya Benjamin Netanyahu, na kwamba watu hawaamini tena propaganda za Waisraeli.

Khawaja Muhammad Asif ametoa maoni hayo kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa X, akipinga matumizi ya tukio la ndege ya Flydubai kwa madhumuni ya propaganda na mkutano wa Netanyahu na mmoja wa abiria Waisraeli wa ndege hiyo.

Aliandika: “Tangu kuanza mashambulizi dhidi ya Gaza, Netanyahu amekuwa akijaribu kuhalalisha simulizi zake kwa kusambaza hadithi za kubuni na kutumia mbinu zisizo na mashiko. Hata hivyo, maoni ya umma duniani yamegeuka kwa nguvu dhidi yake.” Waziri huyo wa Ulinzi wa Pakistan ameongeza kuwa, kulikuwa na kipindi ambacho watu duniani waliamini propaganda za Waisraeli, lakini sasa wamepoteza kabisa uaminifu wao.

Alisema pia: “Huu ni mwelekeo unaoelekea kwenye ukingo wa hatari, na wakati wa kuwajibishwa unakaribia kwa kasi.”

Hali ya taharuki ilitanda ndani ya ndege ya shirika la flydubai iliyokuwa ikitoka Dubai kuelekea Tel Aviv, baada ya rubani msaidizi kumshambulia kwa kisu rubani mkuu akiwa ndani ya chumba cha marubani. Ndege hiyo, iliyokuwa na watu 174, ilianza kupoteza mwinuko kwa kasi baada ya tukio hilo. Rubani mkuu, licha ya kujeruhiwa, alifanikiwa kufungua mlango wa chumba cha marubani, na baadhi ya abiria wakaingia na kumzuia mshambuliaji.

Ndege moja ya Boeing 737 ya kampuni ya Flydubai, ilibadilisha njia yake na kuelekea Saudi Arabia Jumatano iliyopita asubuhi kufuatia mzozo huo.

Uwanja wa Ndege wa Tabuk nchini Saudi Arabia ulitangaza kuwa, baada ya kupokea ujumbe wa dharura kutoka kwenye ndege hiyo, hali ya dharura ilitangazwa uwanjani. Ndege hiyo ilitua salama. Baada ya kutua, rubani na msaidizi wake walipelekwa hospitalini kwa ajili ya kupata matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya utawala wa Israel, ndege hiyo ilikuwa imebeba idadi kubwa ya abiria Waisraeli. Baada ya kutua kwa dharura, mipango ilifanywa ya kuwahamisha abiria hao kwa kutumia ndege nyingine.

Kampuni ya Flydubai nayo ilitangaza baada ya tukio hilo kwamba itasitisha safari zake za ndege kwenda Tel Aviv kwa muda wa siku sita.