SEPAH: Kutimuliwa Wamarekani Iraq ni ishara ya kutimuliwa kwao Asia Magharibi nzima
-
SEPAH: Kutimuliwa Wamarekani Iraq ni ishara ya kutimuliwa kwao Asia Magharibi nzima
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limepongeza kutimuliwa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na kulitaja suala hilo kuwa ni ushindi wa kihistoria na mafanikio makubwa kwa Kambi ya Muqawama.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Jeshi la SEPAH limetoa taarifa likiwakumbuka kwa heshima mashahidi watukufu wa Muqawama wa Kiislamu wa Iraq hasa Shahid Abu Mahdi al-Muhandis na kulipongeza taifa tukufu la Iraq, kambi imara na yenye nguvu ya Muqawama wa Kiislamu, pamoja na wanaopigaa jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na Ulimwengu wa Kiislamu kiujumla, kwa kutimuliwa wavamizi wakiongozwa na Marekani huko Iraq.
Sehemu moja ya taarifa hiyo Jeshi la SEPAH inasema:
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
"Bila ya shaka ahadi yetu ilikwishatangulia kwa waja Wetu, waliotumwa. Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakaonusuriwa."
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, huku likiwaenzi mashahidi watukufu wa Kambi ya Muqawama wa Kiislamu nchini Iraq na eneo la Asia Magharibi hasa Luteni Jenerali Shahid Haj Qasem Soleimani, Shahid Abu Mahdi al-Muhandis na wanamapambano wote waaminifu waliofikia daraja tukufu ya kuuawa shahidi katika miongo miwili ya mapambano dhidi ya Wamarekani wavamizi, linalipongeza taifa tukufu la Iraq, Kambi ya Muqawama wa Kiislalmu na wapiganaji wanamapinduzi wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa ushindi huu wa kihistoria.
Kutimuliwa Marekani nchini Iraq kumetokana na msimamo thabiti wa taifa tukufu la Iraq katika kulinda uhuru wake. Kupitia ustahimilivu wake wa kihistoria, taifa la Iraq limethibitisha kuwa irada na utashi wa kitaifa ndiyo silaha kuu ya kupambana na tamaa ya kupindukia ya madola yenye nia ya kutawala na kukandamiza wengine. Ushindi wa utashi wa mapambano dhidi ya ubabe wa madola hayo uliooneshwa na taifa tukufu la Iraq dhidi ya uvamizi wa Marekani, ni ukurasa wa dhahabu katika historia ya mapambano ya mataifa ya eneo hili katika kupigania uhuru (wao wa kweli). Kutimuliwa Wamarekani wavamizi, kwa hakika, ni utekelezaji wa azimio thabiti la taifa shujaa la Iraq la kupambana na utawala wa kigaidi na wachochezi wa vita yaani Marekani na watawala mabeberu wa Ikulu ya White House. Marekani, ambayo siku zote inatumia lugha ya mabavu, sasa imelazimika kukimbia katika ardhi iliyokuwa ikiikalia kwa mabavu kwa miongo miwili.
Bila shaka, tukio hili tukufu na la kihistoria ni hatua ya kwanza katika kulipiza kisasi cha damu za mashahidi wa Iraq hasa Abu Mahdi al-Muhandis na kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, malipo ya damu yao yatatimia kikamilifu kupitia kufukuzwa kabisa Marekani katika eneo hili zima.
"Na Mwenyezi Mungu hatawapa kamwe makafiri njia [ya kuwashinda] waumini."