Russia yatishia kuwashamblia kwa bomu la nyuklia wanachama wa NATO
Moscow imeionya NATO kwamba inaweza kutumia silaha za nyuklia kuwashambulia wanachama wa jeshi hilo la nchi za Marekani iwapo muungano huo utajaribu kukata mawasiliano kati ya Kaliningrad na eneo kuu la Russia.
Shirika la habari la Mehr limeripoti habari hiyo kupitia Reuters na kusema kuwa, Russia imetuma waraka kwa jeshi la nchi za Magharibi NATO ikilaani chokochoko za muungano huo na kuzitaja kuwa ni hatari kubwa. Imeonya kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya moja kwa moja baina ya Russia na NATO na kusema kuwa, ikilazimika, Moscow haitosita kutumia silaha za nyuklia dhidi ya wanachama wa NATO.
Waraka huo umeeleza kuwa, iwapo nchi wanachama wa NATO zitajaribu kulitenga jimbo la Kaliningrad na kukata mawasiliano baina ya jimbo hilo na maeneo mengine ya Russia, basi Moscow nayo haitosita kutumia uwezo wake wote zikiwemo silaha za nyuklia kulinda eneo hilo na kujihami mbele ya wanachama wa NATO.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, vilevile amesema kuwa, maonyo ya hivi karibuni yaliyotolewa na balozi za Russia katika nchi kadhaa za Ulaya kuhusu jimbo la Kaliningrad la Russia la kuzitaka nchi hizo za Ulaya ziache chokochoko zao za kujaribu kulitenga eneo hilo na maeneo mengine ya Russia, yalikuwa ni kama njia ya kuwakumbusha "watu wenye misimamo mikali barani Ulaya" kuhusu msimamo rasmi wa Moscow.
Kaliningrad ni eneo la Russia lililoko kati ya Poland na Lithuania kwenye pwani ya Bahari ya Baltic.
Katika kujibu onyo hilo la Russia, jeshi la nchi za Magharibi NATO limesema kuwa shughuli na mazoezi yake ya kijeshi si tishio la aina yoyote ile kwa Russia.