SEPAH: Marekani haina tena uwezo wa kuendesha vita kama zamani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141852-sepah_marekani_haina_tena_uwezo_wa_kuendesha_vita_kama_zamani
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzui ya Kiislamu SEPAH amezungumzia hali ya wanajeshi wa Marekani katika eneo hili na kusema kuwa, Marekani hivi sasa haina tena ile hali iliyokuwa nayo kabla ya kuanzisha vita viwili dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-10-01T03:36:01+00:00 )
Oct 01, 2026 03:31 UTC
  • SEPAH: Marekani haina tena uwezo wa kuendesha vita kama zamani

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzui ya Kiislamu SEPAH amezungumzia hali ya wanajeshi wa Marekani katika eneo hili na kusema kuwa, Marekani hivi sasa haina tena ile hali iliyokuwa nayo kabla ya kuanzisha vita viwili dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amesema: Wakati wa "Vita vya Ramadhani" na "Vita vya Siku 12," Wamarekani walikuwa na nafasi ya kipekee; lakini hali hizo zimebadilika na kupungua nguvu hivi sasa.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Brigedia Jenerali Hossein Mohebbi alisema hayo jana Jumatano, Septemba 30 katika kipindi cha "Sobhaneye Irani" (Chai ya Asubuhi ya Iran) katika Kanali ya Pili ya televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 

Msemaji wa SEPAH amejibu swali la mtangazaji aliyeuliza: "Je, kutakuwa na vita vingine au la?" kwa kusema: "Tayari hivi sasa tuko vitani." Amezungumzia pia hali ya wanajeshi wa Marekani katika eneo hili na kusema: "Kwa mtazamo wetu, Marekani haina tena fursa ilizokuwa nazo huko nyuma."

 

"Wakati wa Vita vya Ramadhani na Vita vya Siku 12, Wamarekani walikuwa katika nafasi ya kipekee, kuanzia idadi ya askari wao katika eneo hili, silaha walizokuwa nazo, kambi za kijeshi na matumaini waliyokuwa nayo ya kuilazimisha Iran kusalimu amri, lakini hali hizo zote hivi sasa zimetoweka," amesema.

 

Brigedia Jenerali Mohebbi pia amesema: "Tunaamini kuwa, wanajeshi wa Marekani wamedhoofika na wamekumbwa na uchovu mkubwa, na idadi kubwa ya askari wao wamelazimika kuondoka katika eneo hili."

 

"Hali ya leo ni tofauti na ya zamani; tumezishambulia vikali kambi na vituo vyao vya kijeshi, jambo lililowalazimisha kuwakimbiza wanajeshi wao na kuwapeleka kwenye meli za kubebea ndege za kivita zilizoko umbali wa kwa uchache kilomita 500 kutoka Iran." Kuhusu vituo na vifaa vya Marekani kuwa ndani ya masafa ya mashambulizi ya Iran, msemaji huyo wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Naibu wa Uhusiano wa Umma wa jeshi hilo amesema: "Wamarekani walilazimika kuhamishia mbali na Iran baadhi ya meli na zana zao za kijeshi. Kwa mfano, walihamishia baadhi ya askari wao kwenye kituo cha Al-Kharj, ambacho pia kinafikiwa na mashambulizi ya mashambulizi ya Iran. Vilevile walilazimika kuhamishia wanajeshi na zana zao za kivita kwenye vituo vya Titan, ambavyo navyo pia viko ndani ya masafa ya mashambulizi ya Iran".