Kiongozi wa Mapinduzi: Iran haitarudi tena kamwe kwenye zile zama anazozitamani adui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141796-kiongozi_wa_mapinduzi_iran_haitarudi_tena_kamwe_kwenye_zile_zama_anazozitamani_adui
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei amesema, siku za kutawaliwa na madola ajinabi, ambazo maadui wa Iran wanapigania kuzirejesha, zimeshapita na hazitarudi tena kamwe.
(last modified 2026-09-28T16:40:08+00:00 )
Sep 28, 2026 15:30 UTC
  • Kiongozi wa Mapinduzi: Iran haitarudi tena kamwe kwenye zile zama anazozitamani adui

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei amesema, siku za kutawaliwa na madola ajinabi, ambazo maadui wa Iran wanapigania kuzirejesha, zimeshapita na hazitarudi tena kamwe.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo katika ujumbe aliotoa leo Jumatatu kwa mnasaba wa maadhimisho ya "Wiki ya Kujihami Kutakatifu", inayosadifiana na kumbukumbu ya kuanza kwa vita vilivyoanzishwa na dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein, dhidi ya Iran kati ya mwaka 1980 na 1988, na vilevile kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa pili tangu alipouawa shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, katika zama hizo, bahari mbili kusini mwa Iran zilikuwa kama "uwanja wa michezo" kwa vikosi vya adui, lakini sasa vikosi hivyo haviwezi tena kuthubutu kuvuka mipaka ya Bahari ya Arabia kutokana na vipigo vikali vilivyopata kutoka kwa wapiganaji shupavu wa Iran na walinzi wa Mlango-Bahari wa Hormuz.

Amesema, katika kipindi cha "Kujihamu Kutakatifu" miale inayovukuta ya jua la Mapinduzi iliyosambaa kote nchini Iran ilileta hisia za kupendeza za mshikamano wa kitaifa na utiifu kwa fikra na njia ya Uislamu wa kimapinduzi; hali ambayo ilianza kuyeyusha "barafu ya aina za zamani na mpya za ubeberu na ukoloni."

Ayatullah Khamenei amekumbusha kuwa, "siku zilizopita zilikuwa za giza," wakati ambapo mabalozi wa madola ya kiistikbari walikuwa wakifikisha maagizo yao kwa mfalme wa Iran, ambaye alilazimika kuyatekeleza iwe kwa kupenda au kwa kutopenda.

Amesisitiza kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 yalipindua mfumo huo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, hilo lilikuwa jambo gumu sana kwa madola ya kibeberu yaliyotaka kuitawala Iran na yaliyokuwa yakimezea mate utajiri wa nchi hii, madola ambayo kwa miaka mingi yalifanya dhuluma mbalimbali dhidi ya watu wa taifa hili katika hatua za kujaribu kujimilikisha utajiri huo.

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, Ayatullah Khamenei amesema: “leo hii, baadhi wanatuona kama dola kuu la nne lenye nguvu duniani na bila shaka, wanasema hivyo kwa kuzingatia mahesabu ya kidunia.”

Ameongezea kwa kusema: “hata hivyo, kwa mujibu wa mahesabu ya kidini, nchi inayojichukulia kuwa ni ya wafuasi wa Kizazi Kitoharifu cha Mtume Muhammad SAW, ambayo watu wake wamejitolea kwa dhati kuwatii waja hao watukufu na hawana hofu katika kusimamia ukweli, nchi hiyo inahesabiwa kuwa ndiyo nguvu kuu ya kwanza duniani”.

Katika ujumbe wake huo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amemuenzi kiongozi wa zamani wa Hizbullah ya Lebanon Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kutimia mwaka wa pili tangu kuuawa kwake shahidi, akimwelezea kiongozi huyo wa Hizbullah kama shakhsia shujaa wa Waarabu na nembo kuu ya mhimili wa Muqawama.

Ayatullah Khamenei amesema, Shahidi Nasrullah alikuwa mtu mwenye nia njema na ya dhati kwa watu wake na njia aliyopigania, ambaye hotuba zake zenye kugusa hisia pamoja na vitendo vyake vya kishujaa viliimarisha nyoyo za watu wa Lebanon na wapigania uhuru kote duniani.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kuwa, Shahidi Nasrullah aliliinua jina na hadhi ya Lebanon, nchi ambayo kwa miaka mingi ilichukuliwa kama "ua wa nyuma tu" (usio na umuhimu) wa madola fulani.

Ameongeza kuwa ushindi na mafanikio vilikuwa wenzi wa kudumu wa Shahidi Nasrullah, akisisitiza kwamba "bendera yake ya fahari" sasa hivi iko mikononi mwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassem, ambaye anaiendeleza njia yake kwa ushujaa…/