Wanamgambo 12 wa al-Shabab waangamizwa katika operesheni maalumu nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141772-wanamgambo_12_wa_al_shabab_waangamizwa_katika_operesheni_maalumu_nchini_somalia
Shirika la Taifa la Ujasusi na Usalama la Somalia (NISA) limetangaza kuwa limefanikia kuangamiza wanamgambo 12 wa al-Shabab katika operesheni maalumu iliyofanyika kwenye eneo la kusini-kati la nchi hiyo.
(last modified 2026-09-28T02:56:43+00:00 )
Sep 28, 2026 02:47 UTC
  • Wanamgambo 12 wa al-Shabab waangamizwa katika operesheni maalumu nchini Somalia
    Wanamgambo 12 wa al-Shabab waangamizwa katika operesheni maalumu nchini Somalia

Shirika la Taifa la Ujasusi na Usalama la Somalia (NISA) limetangaza kuwa limefanikia kuangamiza wanamgambo 12 wa al-Shabab katika operesheni maalumu iliyofanyika kwenye eneo la kusini-kati la nchi hiyo.

 

Katika taarifa yake hiyo, NISA imesema kuwa, operesheni hiyo imefanyika kwenye kijiji cha Bur Saruur, takriban kilomita 2 kusini-mashariki mwa eneo la Ali-Gaduud la mkoa wa Shabelle ya Kati, na kufanikiwa kuharibu maficho pamoja na vifaa vya kijeshi vya magaidi hao.

"Operesheni hiyo imeendeshwa kulingana na mpango maalumu, na msako dhidi ya wanamgambo waliosalia wa al-Shabab unaendelea," limesema shirika hilo la ujasusi katika taarifa iliyotolewa huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Vikosi vya serikali ya Somalia vikisaidiwa na washirika wa kimataifa, vimeongeza kasi ya operesheni zao za kijeshi dhidi ya al-Shabab katika maeneo ya kati na kusini mwa nchi hiyo. Operesheni hizo za pamoja zimepelekea kukombolewa maeneo kadhaa muhimu ya kimkakati na kuharibiwa maficho na maghala ya silaha ya waasi, huku wanajeshi wa Somalia wakiendelea kuwasaka wanamgambo waliosalia.

Mwishoni mwa mwaka jana 2025, wataalamu wa Umoja wa Mataifa walitahadrharisha kwamba genge lenye misimamo mikali la al Shabab bado ni tishio kubwa kwa amani na utulivu nchini Somalia na katika eneo zima pa Pembe ya Afrika ikiwa ni pamoja na katika nchi jirani ya Kenya.

Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ilieeleza kuwa wanamgambo wa al Shabab bado wana uwezo wa kufanya mahambulizi licha ya mafanikio makubwa liliyopata jeshi la Somalia na madola ya kigeni katika kuliangamiza genge hilo la kigaidii.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukirefusha mara kwa mara muda wa kuhudumu kikosi cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (AU) huko Somalia na mwishoni mwa mwaaka jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliongeza muda huo hadi Disemba 31 mwaka huu wa 2026.