Nasrullah; shahid aliyeifufua na kuibakisha hai kadhia ya Palestina
-
Nasrullah; shahid aliyeifufua na kuibakisha hai kadhia ya Palestina
Katika kipindi cha usaliti mkubwa uliofanywa na baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu walioamua kuitelekeza kadhia muhimu ya Waislamu yaani Palestina na kuungana na adui Mzayuni, shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, aliyekuwa Katibu MKuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon hakuitelekeza Ghaza bali alikubali kumwaga damu yake kuwatetea ndugu zake wa Palestina.
Shirika la Habari la Tasnim limeandika makala maalumu kwa mnasaba wa hauli na kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kuuawa shahidi mwanachuoni huyo wa Kishia, chini ya kichwa cha maneno "Bwana wa Mashahidi wa Muqawama; Sayyid Hassan Nasrullah" na kusema, alijitolea kila kitu chake — maisha yake, watoto wake, marafiki zake wa karibu na vijana bora wa Hizbullah — kwa ajili ya kadhia ya Palestina. Alikabidhi kila alichokuwa nacho kwenye suala muhimu zaidi kwa ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu yaani kadhia ya Palestina, na hatimaye akafikia daraja ya juu na tukufu ya kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Sehemu nyingine ya makala hiyo imesema: Vita vya kikatili na vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza mwezi Oktoba 2023 ukisaidiwa kikamilifu na Marekani na madola makubwa ya Magharibi, vilifichua mambo mengi ikiwa ni pamoja na unafiki wa baadhi ya watawala wa nchi za Waislamu lakini pia imani ya kweli na thabiti ya Kambi ya Muqawama.
Mwandishi wa makala hiyo anaendelea kuandika: Wengi wanaamini kwamba kama Hizbullah ingeliwatelekeza Wapalestina na kuiacha peke yake Ghaza, huenda Shahid Sayyid Hassan Nasrullah angelikuwa amebaki hai kimwili, lakini bila ya shaka yoyote angelikuwa amekufa kikamilifu katika nyoyo za Wapalestina na wapigania haki dunia na angelipoteza kabisa heshima na hadhi yake kubwa miongoni mwao.
Lakini alifanya lililo la busara na chaguo bora kabisa, la kutowaacha peke yao Waislamu wenzake wa Palestina na aliingia haraka kuwanusuru. Kuingia Hizbullah katika vita hivyo kuliifufua kadhia ya Palestina na kuibakisha hai hadi hivi sasa, adui Mzayuni alishughulishwa kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel na hivyo kuwapa mwanya Wapalestina wa Ghaza kujipanga vizuri zaidi kukabiliana na jinai za kutisha za Israel.