Iran yatengeneza chanjo za wanyama wa majini kwa kutegemea teknolojia ya ndani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141752-iran_yatengeneza_chanjo_za_wanyama_wa_majini_kwa_kutegemea_teknolojia_ya_ndani
Watafiti wa Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu ya Tehran wamefanikiwa kupata ujuzi wa kiteknolojia wa kutengeneza chanjo za wanyama wa majini.
(last modified 2026-09-27T03:00:59+00:00 )
Sep 27, 2026 02:59 UTC
  • Iran yatengeneza chanjo za wanyama wa majini kwa kutegemea teknolojia ya ndani

Watafiti wa Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu ya Tehran wamefanikiwa kupata ujuzi wa kiteknolojia wa kutengeneza chanjo za wanyama wa majini.

Mafanikio hayo yanaweza kuiwezesha Iran kujitosheleza kwa chanjo hizo na kuondokana na utegemezi wa uagizaji kutoka nje ya nchi.

Kikundi cha utafiti wa bidhaa za kibaolojia za mifugo cha Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu ya Tehran kilianza kufanya utafiti kuhusu chanjo za wanyama wa majini mwaka 2005. Mwaka 2014, kilipata kibali chake cha kwanza kutoka Shirika la Mifugo la Iran cha kutengeneza chanjo dhidi ya ugonjwa wa streptokokasi (streptococcosis).

Mwaka 2017, kikundi hicho kilipata kibali cha pili cha kutengeneza chanjo ya samaki dhidi ya ugonjwa wa yersiniosis. Chanjo zilizotengenezwa na Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu ya Tehran zilianza kutumika katika mashamba ya ufugaji wa samaki nchini Iran tangu mwaka 2014, na timu ya wataalamu wa kikundi hicho ilipata uzoefu mkubwa katika utoaji wa chanjo kwa samaki.

Tangu mwaka 2015, uzalishaji wa chanjo pia ulianza kufanyika kwa ushirikiano na kampuni ya Iran inayotegemea maarifa na teknolojia. Tangu wakati huo, kwa msaada wa kitaalamu kutoka kwa kikundi cha utafiti, chanjo za samaki zimetengenezwa na kusambazwa na kampuni hiyo.

Watafiti wa Jihad ya Vyuo Vikuu ya Tehran walianza pia kufanya utafiti kuhusu chanjo za samaki wa baharini mwaka 2017. Katika hatua hiyo, waliwasiliana na mashamba ya ufugaji wa samaki kwenye vizimba vilivyoko kusini mwa Iran na kuchukua sampuli za bakteria kutoka katika mashamba hayo. Sampuli hizo zilitumika kutengeneza chanjo za awali, ambazo baadaye zilifanyiwa majaribio katika mashamba ya ufugaji.

Kupitia tafiti hizo, watafiti walifanikiwa kupata ujuzi wa kiteknolojia wa kutengeneza chanjo dhidi ya magonjwa ya streptococcosis na vibriosis yanayowapata samaki aina ya sea bass. Kwa sasa, kupata kibali cha uzalishaji wa chanjo hizo ni miongoni mwa mipango ya kikundi cha utafiti wa bidhaa za mifugo cha Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu ya Tehran.