EU lazima iwajibishwe kwa uvamizi wa Marekani nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141732-eu_lazima_iwajibishwe_kwa_uvamizi_wa_marekani_nchini_iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Ulaya na wanachama wa NATO lazima wawajibishwe kwa uvamizi wa Marekani dhidi ya Iran.
(last modified 2026-09-26T03:30:13+00:00 )
Sep 26, 2026 03:28 UTC
  • EU lazima iwajibishwe kwa uvamizi wa Marekani nchini Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Ulaya na wanachama wa NATO lazima wawajibishwe kwa uvamizi wa Marekani dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Esmaeil Baghaei ameandika hayo kwenye mtandao wa X usiku wa kuamkia leo Jumamosi akijibu kauli za Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, kuhusu kushiriki kwa kiwango kikubwa nchi za Ulaya na wanachama wa NATO katika uvamizi wa kijeshi wa Marekani na Israel nchini Iran.

Baghaei amesema kuwa matamshi hayo ya Rutte ya kwamba Marekani alitumia kwa kiwango kikubwa vituo vilivyoko Ulaya kufanya maandalizi na kuendesha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran, ni kukiri wazi kwamba Ulaya ilishiriki kwa makusudi na kikamilifu katika vita hivi haramu. Kukiri huku kunakinzana kabisa na kukanusha kwao mara kwa mara kuhusika katika kipindi chote cha mgogoro huo.

Ameongeza kwa kuandika: Umoja wa Ulaya, nchi wanachama wake na wanachama wa NATO lazima wawajibishwe kwa kushiriki katika uvamizi huo wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran. Hii inajumuisha kuwajibika kwa aina yoyote ya uungaji mkono wa kisiasa, kijeshi, kilojistiki au aina nyinginezo zote zilizochangia mauaji na uharibifu ndani ya Iran pamoja na madhara yanayoendelea hadi hivi sasa. Raia wa Ulaya wana haki ya kudai majibu ya maswali yao kutoka kwa serikali zao kuhusu maamuzi yaliyochukuliwa ya kuunga mkono au kushiriki katika uvamizi huo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amesema: Kupanda vibaya bei ya mafuta na madhara mengine ya vita hivi haramu, lazima lawama zake zibebwe na serikali za Ulaya kwa maamuzi maovu ziliyochukua yaliyowezesha kufanyika uvamizi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Aidha amesisitiza  kuwa nafasi ya Mark Rutte kama Katibu Mkuu wa NATO ikiwemo hatua na maamuzi yaliyochukuliwa wakati wa uongozi wake kuhusu vita hivi haramu, nayo pia lazima ichunguzwe.