Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa: Jukwaa la Iran Kudai Haki
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Mwaka huu, Umoja wa Mataifa utatumika kama jukwaa la kuelezea masaibu yanayowakabili wananchi wa Iran, mashahidi wa shule ya Minab na Kiongozi Mkuu aliyeuawa shahidi."
Kauli hii ya Seyed Abbas Araghchi iliashiria mwelekeo wa vikao na hotuba za ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, kama ilivyothibiti katika hotuba kali iliyotolewa na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran katika Baraza Kuu la umoja huo siku ya Jumatano mchana kwa wakati wa New York. Ujumbe wa Iran umekwenda New York mwaka huu kutangaza ukweli ulio wazi: Marekani na utawala wa Kizayuni zilifanya uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran, na taifa la Iran ndilo lililobeba gharama na madhara ya mashambulizi hayo. Kwa Iran, vita hivi havikuwa vya kichokozi tu dhidi ya mfumo wa Kiislamu bali umekuwa mtihani mkubwa kwa mfumo wa kimataifa. Iran inatetea ardhi yake katika uwanja wa vita, na sasa imefika mjini New York kwa ajili ya kutetea ukweli kuhusu vita hivi katika uwanja wa diplomasia.
Araghchi ameongeza kuwa vita bado vinaendelea, hivyo safari ya ujumbe wa Iran mjini New York haijakuwa safari ya kawaida tu ya kidiplomasia. Jitihada endelevu za Iran za kujitetea zinafanyika katika nyanja tofauti, wakati huu, katika Umoja wa Mataifa, mbele ya fikra za waliowengi duniani na katika vyombo vya habari vya kimataifa. Ni uwanja wa mapambano ya kudhihirisha ukweli na kuzuia juhudi za kupotoshwa kwake. Mstari wa mbele wa mapambano haya ya haki dhidi ya batili unaongozwa na Ayatullah Khamenei Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyeuawa shahidi kidhulma na magaidi wakiongozwa na Marekani. Kuuawa shahidi kiongozi wa taifa wakati wa uchokozi wa kijeshi si jambo linaloweza kutenganishwa na muktadha mpana wa vita. Tukio hili ni sehemu ya uhalisia mchungu wa vita vya kichokozi vinavyoendeshwa dhidi ya wananchi wa Iran. Shambulio la adui dhidi ya shule ya Minab nalo ni sehemu muhimu ya uhalisia huo. Watoto na walimu 168 wasio na hatia waliuawa kinyama katika tukio hilo la kigaidi, watoto ambao walikuwa darasani, na si katika uwanja wa vita. Kuuawa shahidi kwao si takwimu tu, bali ni jinai ambayo wahusika wake wanapaswa kuwajibishwa kisheria. Katika muktadha huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameuuliza swali zito Umoja wa Mataifa: Je, imani iliyopotea kwa taasisi hii inaweza kurejeshwa?
Kurejesha imani kwa Umoja wa Mataifa ndiyo kaulimbiu ya Mkutano Mkuu wa mwaka huu. Wito huu unatolewa wakati ambapo uaminifu kwa taasisi za kimataifa unakabiliwa na mashinikizo makubwa. Imani hupungua pale uchokozi wa kijeshi unapofanyika na jamii ya kimataifa kuamua kukaa kimya au kutoa jibu dhaifu lisiloendana na ukubwa wa uchokozi wenyewe. Imani huporomoka pale uteteaji wa haki za binadamu unapofanywa kwa upendeleo. Itibari ya sheria za kimataifa hupotea pale sheria kali zinapotekelezwa dhidi ya baadhi ya mataifa huku mengine yakifumbiwa macho na kutochukuliwa hatua zinazofaa. Hii ndiyo hali hasa inayoikabili Iran. Kwa nini sheria za kimataifa zinatekelezwa kidhulma dhidi ya watu wa Iran huku wangine wakiruhusiwa kuzikiuka hadharani bila kuchukuliwa hatua yoyote?
Ni matarajio ya wengie kuwa maswali haya muhimu yatapata majibu yanayofaa katika mijadala ya kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York. Iran haitaki kuacha suala la uchokozi wa kijeshi dhidi yake lizame katika mtiririko wa habari za kila siku duniani, wala kusahaulika mashahidi wa shule ya Minab. Haiko tayari kuona mauaji ya kikatili yaliyofanywa dhidi ya Kiongozi Mkuu wake yakichukuliwa kama tukio la kawaida tu katika historia ya vita. Tehran imesisitiza kuwa harakati za taifa la Iran za kutafuta haki bado zinaendelea. Hivyo, shughuli nyingi za Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, na ujumbe anaoandamana nao mjinji New York ikiwemo hotuba yake katika Baraza Kuu, mahojiano na vyombo vya habari, mikutano na viongozi mbalimbali wa dunia, pamoja na vikao vya kimataifa, zote hizo zina lengo moja tu: Kufikisha ujumbe na mtazamo wa Iran kwa ulimwengu.
Hii ni diplomasia inayolenga kupigania haki na ukweli. Taifa la Iran limesimama imara dhidi ya uchokozi wa adui. Limetoa wahanga wengi mashahidi na kubeba gharama kubwa, lakini pamoja na hayo halijakata tamaa na wala halitasalimu amri mbele ya adui. Viongozi wa Iran wamefika New York ili kuwa sauti ya wale ambao hawawezi tena kujitetea wenyewe. Sauti ya mashahidi wa shule ya Minab, sauti ya Kiongozi Mkuu aliyeuawa shahidi, sauti ya familia zilizofiwa, na sauti ya taifa linalotangaza kuwa ukweli kuhusu vita hauwezi kufichwa wala kupotoshwa.
Mwaka huu, Umoja wa Mataifa unazungumzia madai ya kurejesha imani iliyopotea. Lakini Iran nayo ina jibu la wazi kuhusu madai hayo: Imani hairejeshwi kwa kaulimbiu na maneno matupu; inarejeshwa kupitia vitendo na watu kutendewa haki. Inarejeshwa kupitia utekelezaji wa sheria kwa usawa. Inarejeshwa kwa kumuwajibisha mchokozi. Hivyo, kwa Iran, New York mwaka huu ni jukwaa la kutetea haki, jukwaa kwa ajili ya kutendewa haki mashahidi wa Iran na kwa ajili ya kusema ukweli kuhusu vita vilivyolazimishwa dhidi ya taifa hili linalodhulumiwa na nchi zenye kiburi duniani, zinazokanyaga sheria hadhari bila kuwajibishwa na yeyote yule.