Hamas: Lengo la utawala wa Israel ni kuhitimisha shughuli za UNRWA
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema: Lengo la utawala wa Israel katika ni kukomesha shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA).
Hazem Qassem amesema, utawala vamizi wa Israel inataka kuzuia kikamilifu shirika hilo kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Palestina, na kuondoa haki ya wakimbizi wa Palestina kurejea katika maeneo yao. Ameongeza kuwa msimamo uliotangazwa na Baraza la Amani pia unaelekea katika mwelekeo huo huo.
Hazem Qassem, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hamas, amesema hayo akijibu msimamo wa Baraza la Amani kuhusu Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA.
Msemaji huyo wa Hamas ameuelezea uamuzi wa Baraza la Amani wa kutoshirikiana na UNRWA na kuliona shirika hilo kuwa halina nafasi kama msimamo unaoendana kikamilifu na msimamo pamoja na matakwa ya utawala wa Israel.
Amesisitiza kwamba lengo la utawala wa Israel katika msimamo huo ni kukomesha shughuli za UNRWA, kuzuia shirika hilo kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Palestina, na kuondoa haki ya wakimbizi wa Palestina kurejea katika maeneo yao.
Msemaji huyo wa Hamas pia amesema ni jambo la kushangaza kwamba Baraza la Amani linachukua msimamo wa uhasama dhidi ya UNRWA, wakati baraza hilo lenyewe linashindwa kutoa misaada ya kibinadamu kwa Gaza au kuishinikiza Israel kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na kukomesha mauaji ya kila siku dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Hivi majuzi Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) sanjari na kusisitiza utayari wake kamili wa kutekeleza ramani ya njia iliyokubaliwa na ofisi ya Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mpango wa amani wa Gaza, ilionya kuwa kuvunjika kabisa makubaliano ya kusitisha mapigano na ramani hiyo ya njia kunatokana na utawala unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina kukataa kuheshimu makubaliano hayo.