Ebola yaua wanafunzi 10 DRC wakati mlipuko ukiongezeka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i142230-ebola_yaua_wanafunzi_10_drc_wakati_mlipuko_ukiongezeka
Angalau wanafunzi 10 wameuawa na ugonjwa wa virusi vya Ebola katika mkoa wa Ituri ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2026-10-16T09:19:26+00:00 )
Oct 16, 2026 09:17 UTC
  • Ebola yaua wanafunzi 10 DRC wakati mlipuko ukiongezeka

Angalau wanafunzi 10 wameuawa na ugonjwa wa virusi vya Ebola katika mkoa wa Ituri ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hii inajiri zaidi ya mwezi mmoja tangu shule zilipofunguliwa kwa ajili ya mwaka mpya wa masomo huku mlipuko ukiendelea.

Takwimu zilizotolewa Alhamisi na maofisa wa elimu katika mji mkuu wa mkoa huo, Bunia, zilionyesha kuwa waliofariki ni miongoni mwa kesi 25 zilizothibitishwa za Ebola, ambazo zimerekodiwa miongoni mwa wanafunzi katika shule kadhaa mkoani humo.

Wanafunzi kumi kati ya wale walioambukizwa wamefariki huku saba wakiwa wanapata matibabu katika vituo maalum vya Ebola mkoani humo.

Ofisa wa elimu wa mkoa, Yvon Muke, amezihimiza shule kuimarisha hatua za kuzuia ili kupunguza kuenea kwa virusi hivyo ndani ya shule.

Muke alisema serikali, kwa ushirikiano na wadau wa kimataifa, inaongeza juhudi za kupambana na janga hilo mashuleni kwa kusambaza viuatilifu na vifaa vya kujikinga kwa ajili ya wanafunzi na wafanyakazi.

Ofisa huyo alizihimiza shule kuhakikisha matumizi sahihi ya vifaa hivyo na kufuata maagizo ya afya ili kupunguza hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo.

Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, katika ripoti ya hali ya mambo Jumatano, ilisema mlipuko nchini Kongo unaendelea kubadilika, ukipanuka kijiografia na kwa upande wa maambukizi na vifo.

Janga la hivi karibuni limeathiri kanda 65 za afya katika mikoa saba ambayo ni Haut-Uele, Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Bas-Uele, Tshopo, na Ubangi Kusini.

Ituri inasalia kuwa kitovu kikuu cha mlipuko huo, wakati maambukizi makubwa yakiendelea kushuhudiwa Kivu Kaskazini na Haut-Uele.

Idadi ya kesi zilizothibitishwa nchini Kongo imefikia 9,144, ikiwa ni pamoja na vifo 4,410 tangu kutangazwa kwa mlipuko huo mwezi Mei, kulingana na taarifa mpya ya Wizara ya Afya.