Ripoti: Utawala wa Trump wajaribu kumvua uraia Mbunge Ilhan Omar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i142204-ripoti_utawala_wa_trump_wajaribu_kumvua_uraia_mbunge_ilhan_omar
Utawala wa Trump unamchunguza Mbunge Ilhan Omar wa chama cha Democratc kutoka jimbo la Minnesota, katika hatua inayodaiwa kuwa na lengo la kuandaa mazingira ya kumvua uraia wa Marekani na kisha kumfukuza nchini humo.
(last modified 2026-10-15T11:34:40+00:00 )
Oct 15, 2026 11:30 UTC
  • Ripoti: Utawala wa Trump wajaribu kumvua uraia Mbunge Ilhan Omar

Utawala wa Trump unamchunguza Mbunge Ilhan Omar wa chama cha Democratc kutoka jimbo la Minnesota, katika hatua inayodaiwa kuwa na lengo la kuandaa mazingira ya kumvua uraia wa Marekani na kisha kumfukuza nchini humo.

Mbunge huyo mzaliwa wa Somalia wa chama cha Democratic amekuwa akishambuliwa kwa maneno makali ya mara kwa mara na Rais Donald Trump wa Marekani na Warepublican bungeni.

Idara ya Usalama wa Taifa sasa inamlenga kwa sababu za kisiasa kama sehemu ya njama za utawala wa Trump za kukandamiza upinzani, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani na watu wengine wanaofahamu vizuri uchunguzi huo, uliofichuliwa na gazeti la Wall Street Journal.

Siku ya Jumatatu, mawakala wa Usalama wa Marekani walivamia nyumba yake huko Washington, DC, na kumnyang'anya simu yake ya mkononi, daftari, kompyuta binafsi na pasipoti. Uchunguzi unaendelea kuhusu mchakato uliotumika kumpa Omar mwenye umri wa miaka 44 uraia wa Marekani.

Familia ya Omar, ambayo iliishi kwa miaka minne katika kambi ya wakimbizi nchini Kenya, ilipewa hadhi ya ukimbizi nchini Marekani na kuwasili mjini New York mwaka 1995. Hata hivyo, ilichukua miaka mitano mingine kabla ya yeye kukubaliwa kuwa raia wa Marekani akiwa na umri wa miaka 17.

Uchunguzi huo unalenga kuchunguza historia ya uhamiaji ya mbunge huyo ili kubatilisha uraia wake na kumfukuza nchini, kulingana na ripoti ya gazeti la WSJ.

Hatua hiyo ya upekuzi imechukuliwa wakati zikiwa zimesalia takriban wiki tatu tu kabla ya kufanyika uchaguzi wa katikati ya muhula, ambapo anawania kuchaguliwa tena.

Mtu mmoja mwenye ufahamu wa mchakato huo ameliambia gazeti la WSJ, kuwa wtu wapatao 12, wakiwemo baadhi ya ndugu za Omar, tayari wametakiwa kwenda kutoa ushahidi mbele ya Baraza Kuu la Mahakama ya Shirikisho huko Minnesota.

Mumewe Omar, Tim Mynett, naye pia anafutiliwa kama sehemu ya uchunguzi huo. Omar ameendelea kusimama imara na kuikosoa vikali serikali ya Trump kwa kutoa madai ya uongo. Ameelezea hatua hiyo kama jaribio la utawala wa Trump la kuwatisha wapinzani wa kisiasa kupitia kampeni za kuwachafulia jina, akisisitiza kuwa hatanyamazishwa.