Maandamano yanaendelea nchini Ufaransa sambamba na ukatili wa polisi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i142208-maandamano_yanaendelea_nchini_ufaransa_sambamba_na_ukatili_wa_polisi
Maandamano yanayoendeshwa na wanafunzi wa shule za sekondari nchini Ufaransa, yakiungwa mkono na makundi mbalimbali, wakiwemo walimu, wafanyakazi, wanafunzi wa vyuo vikuu na hata baadhi ya wanasiasa, yangali yanaendelea.
(last modified 2026-10-15T11:49:18+00:00 )
Oct 15, 2026 11:43 UTC
  • Maandamano yanaendelea nchini Ufaransa sambamba na ukatili wa polisi

Maandamano yanayoendeshwa na wanafunzi wa shule za sekondari nchini Ufaransa, yakiungwa mkono na makundi mbalimbali, wakiwemo walimu, wafanyakazi, wanafunzi wa vyuo vikuu na hata baadhi ya wanasiasa, yangali yanaendelea.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, wanafunzi wa shule za sekondari katika miji mbalimbali ya Ufaransa waliingia mitaani tena siku ya Jumanne, ikiwa ni wiki ya tatu ya maandamano yao. Maandamano hayo yaliyoenea katika miji mikubwa ya Ufaransa, kama ilivyokuwa katika siku chache siku zilizopita, yaliambatana na vitendo vya vurugu na mapambano yaliyohusisha polisi.

Kulingana na muungano wa vyama vya wanafunzi na wanafunzi wa shule za sekondari nchini Ufaransa, takriban watu 480,000 walishiriki katika maandamano ya karibuni kote nchini humo, huku Wizara ya Mambo ya Ndani ikitoa takwimu ya watu 161,500. Polisi walieleza kuwa mjini Paris, watu 41,500 waliingia mitaani katika maandamano mawili tofauti.

Vitendo vya vurugu vilivyofanywa na polisi dhidi ya waandamanaji, ambapo wengi wao ni watoto walio chini wa umri wa kisheria, vinaendelea kuzua wasiwasi na hisia kali kimataifa. Wakati huo huo, gazeti la Ufaransa la Le Figaro, liliripoti siku ya Jumanne kuwa karibu watu 1,000 wamewekewa vizuizini kusini mwa Ufaransa pekee; wengi wao wakiwa ni watoto, na kwamba ni mara yao ya kwanza kukabiliwa na ukandamizaji wa polisi.

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa imetangaza kuwa tangu kuanza kwa maandamano ya wanafunzi wa shule za sekondari mnamo tarehe 18 Septemba, "karibu maafisa wa polisi 900," wanafunzi zaidi ya 200, na wafanyakazi 147 wa Wizara ya Elimu ya Taifa wamepata majeraha.