Tukio la polisi kumpiga risasi mwanamke lazusha machafuko Mauritius, skuli zafungwa
Serikali ya Mauritius imezifunga skuli katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kufuatia machafuko yaliyozuka usiku wa kuamkia Jumanne, baada ya polisi kumpiga risasi msichana mmoja.
Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimetangaza kuwa, sajenti wa polisi amefunguliwa mashtaka kuhusiana na tukio la kumpiga risasi Élodie Thomas, mwenye umri wa miaka 27.
Hata hivyo, taarifa hizo hazikueleza kwa kina kilichosababisha tukio hilo.
Thomas alijeruhiwa kwa risasi Ijumaa usiku alipokuwa kwenye gari akirudi nyumbani kutoka kazini, katika eneo la makazi lililopo kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Port Louis.
Waziri wa Afya, Anil Bachoo, amesema Thomas alifanyiwa upasuaji na kutolewa risasi iliyokuwa mwilini mwake.
Polisi bado hawajatoa maelezo rasmi kuhusu tukio hilo, lakini wamethibitisha kuwa uchunguzi unaendelea.
Usiku wa Jumatatu, waandamanaji walichoma moto matairi na kufunga barabara katika baadhi ya maeneo, hali iliyopelekea polisi kupelekwa katika maeneo yaliyoathirika kudhibiti hali ya usalama.
Kutokana na vurugu hizo, mitihani ya tathmini ya wanafunzi iliyopangwa kufanyika Jumanne, Oktoba 13, iliahirishwa hadi tarehe nyingine.
Wizara ya Elimu ilitangaza kuwa skuli za maandalizi, za msingi na za sekondari zingefungwa siku nzima jana Jumanne, Oktoba 13.
Aidha, wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu walielekezwa kuendelea na masomo kwa njia ya mtandao, ambapo
mihadhara yote iliyopangwa kufanyika siku hiyo ilifanyika kwa njia hiyo.
Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema hali ya usalama nchini humo imerejea katika hali ya kawaida na kwamba huduma zote za sekta ya umma zitaendelea kutolewa kama kawaida.
Machafuko ya aina hiyo si ya kawaida katika kisiwa hicho kilichoko katika Bahari ya Hindi kusini mashariki ya bara la Afrika.
Hata hivyo, Wizara ya Elimu haikutaja tarehe ambayo skuli zitafunguliwa tena, ikisema itatoa taarifa zaidi baadaye…/