Kabila azindua muungano mpya wa kisiasa-kijeshi nchini DRC, kupambana na serikali
Joseph Kabila, rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC amezindua muungano mpya wa kisiasa na kijeshi kuchukua nafasi ya kundi la AFC-M23 linalopigana dhidi ya serikali kuu ya Kinshasa, katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo. Hatua yake hiyo inamfanya kuwa na ushiriki wa moja kwa moja katika uasi ambao amekuwa akijiepusha kuunga mkono hadharani.
Kundi hilo jipya linalojiita FRN litaongozwa moja kwa moja na Kabila mwenyewe akisaidiwa na Corneille Nangaa, Bertrand Bisimwa, Freddy Kaniki na Sultani Makenga.
Viongozi wa Congo Kinshasa wamekuwa wakimtuhumu Kabila kwa muda mrefu kuwa anaunga mkono kundi la AFC/M23, ambalo mwaka uliopita liliteka eneo kubwa mashariki mwa Congo, lakini akikanusha vikali jambo hilo.
Akitoa hutuba siku ya Ijumaa, rais huyo wa zamani wa DRC iliituhumu serikali ya Kinshasa kwa kuhusika na vitendo vya ufisadi, utawala mbaya na kushindwa jeshi la taifa mashariki mwa Congo, pamoja na kupinga miamala ya madini ya serikali na utawala wa Marekani. Kabila ni mshirika wa Nangaa, mkuu wa zamani wa Tume ya Uchaguzi ya Congo ambaye alisimamia uchaguzi wenye utata wa 2018 ambao ulimwingiza madarakani Rais Felix Tshisekedi wa sasa na kumaliza kipindi cha utawala wa Kabila.
Umoja wa Mataifa na serikali za Magharibi zinaituhumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23, jambo ambalo linakanushwa na serikali ya Kigali. Kabila alihukumiwa kifo na mahakama ya kijeshi bila yeye mwenyewe kuwa mahakamani, kwa tuhuma za usaliti, jinai za kivita na dhidi ya binadamu kwa kuunga mkono vitendo vya AFC/M23, mashariki mwa Congo, tuhuma ambazo alizikanusha, akisema alielekezewa tuhuma hizo kwa sababu za kisiasa.