Netanyahu aishinikiza Saudi Arabia imruhusu ajiunge na uvamizi dhidi ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i142158-netanyahu_aishinikiza_saudi_arabia_imruhusu_ajiunge_na_uvamizi_dhidi_ya_yemen
Inaripotiwa kuwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, anatafuta idhini ya Saudi Arabia, kupitia ushawishi wa Marekani, ili utawala huo uruhusiwe kushiriki moja kwa moja katika hujuma inayofanywa na utawala wa Riyadh dhidi ya taifa la Yemen.
(last modified 2026-10-13T11:43:30+00:00 )
Oct 13, 2026 11:41 UTC
  • Netanyahu aishinikiza Saudi Arabia imruhusu ajiunge na uvamizi dhidi ya Yemen

Inaripotiwa kuwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, anatafuta idhini ya Saudi Arabia, kupitia ushawishi wa Marekani, ili utawala huo uruhusiwe kushiriki moja kwa moja katika hujuma inayofanywa na utawala wa Riyadh dhidi ya taifa la Yemen.

Kulingana na ripoti ya gazeti la Haaretz, inasemekana kuwa Netanyahu anaona hatua hiyo kama njia nzuri zaidi ya kuimarisha uhusiano na Riyadh na kuandaa mazingira ya kuhalalisha uhusiano huo katika siku zijazo.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa Mohammed bin Salman Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia anapinga ombi hilo kutokana na hofu ya kuchochea malalamiko au upinzani wa umma wa Kiislamu, ambapo bila ya idhini yake akiwa Waziri Mkuu wa ufalme huo, kuna uwezekano mdogo kwa Israel kupata ruhusa ya kushiriki katika vita hivyo. Saudi Arabia imedai mara kwa mara kuwa itarasimisha uhusiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel pale tu taifa la Palestina litakapokuwa limeanzishwa, jambo ambalo Netanyahu ameahidi kulizuia kwa kila njia katika kauli zake za hivi karibuni za kampeni za uchaguzi.

Matukio haya yanajiri huku jeshi la Yemen likipanua uwepo wake katika pwani ya magharibi na kuzingira Lango-Bahari la kimkakati la Bab al-Mandeb, pamoja na kuyakomboa maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa hapo awali na vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia.

Utawala wa Sana’a ulitangaza kuzuia usafiri wa majini dhidi ya Saudi Arabia tarehe 20 Julai, ikiwa ni hatua ya kujibu "mzingiro usio halali na wa kidhalimu" uliowekwa na Saudia dhidi ya Yemen, uliodumu kwa karibu miaka 12.

Jeshi la Yemen limetangaza kufanikiwa kwa operesheni kadhaa zilizolenga meli zinazohusishwa na Saudi Arabia katika Bahari Nyekundu.

Mnamo Machi 2015, Saudi Arabia na washirika wake waliweka mzingiro dhidi ya Yemen na kuanzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi, wakipata uungaji mkono wa kijeshi, kisiasa, na kioperesheni wa Marekani na nchi kadhaa za Magharibi.

Jambo hilo limesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya raia wa Yemen. Hata hivyo, Saudi Arabia imeshindwa kufikia lengo lake lililotangazwa rasmi la kurejesha nchini humo utawala wa kibaraka unaotumikia maslahi yake.

Kundi la Ansarullah la Yemen limeapa kuwa vikosi vya jeshi la nchi hiyo vitaendelea kuongeza ukubwa wa operesheni zake ndani kabisa ya ardhi ya Saudi Arabia, na kushikilia msimamo wa "mzingiro kwa mzingiro na hatua kali kwa hatua kali," hadi pale uchokozi dhidi ya Yemen utakapokomeshwa na mzingiro huo kuondolewa kabisa.