Spika: Marekani lazima iadhibiwe, ikubali matakwa halali ya taifa la Iran
Spika wa Bunge, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema Marekani lazima iadhibiwe kwa vitendo vyake vya kikatili dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku akisisitiza kuwa Tehran inalenga kujenga "ngao ya kudumu kuhofisha hujuma".
Qalibaf amesisitiza: "Marekani lazima iadhibiwe, ibadili tabia yake, na ifanywe ielewe bila shaka yoyote kwamba lazima ikubali matakwa halali ya taifa la Iran".
Spika wa Bunge amebainisha kuwa, mkakati wa Iran hauhusishi kuendeleza vita visivyo na mwisho wala kufanya mazungumzo ya kudumu, bali unahusisha kutumia nguvu za kijeshi na diplomasia ili kulazimisha upande pinzani ukubali matakwa yake.
Qalibaf amesema, Iran inapaswa ipambane kwa nguvu zake zote pale inapobidi, iimarishe utayari wake, na kuugeuza ushindi wa kijeshi kuwa mafanikio ya kisiasa.
“Ili kufanikisha hili, tutapambana na tutafanya mazungumzo pia. Hii ina maana kwamba, inapobidi, ni lazima tupambane kwa nguvu zetu zote, tutumie kila fursa kuimarisha utayari wetu, na kila tunapopata ushindi wa kijeshi kwenye uwanja wa vita, tuugeuze kuwa ushindi wa kisiasa pia, tuuzatitii, na kuufanya uwe ushahidi wa kushindwa kwa adui,” amefafanua Spika wa Bunge la Iran na akaongezea kwa kusema: “kwenye medani ya vita, mbele ya Mwenyezi Mungu, ni lazima tuamini kuwa tunapaswa kupambana kwa ujasiri dhidi ya adui yetu anayetumia mabavu kutulazimisha, huku pia tukishiriki katika mazungumzo ili kujenga uwezo na ngao ya kudumu ya kuhofisha hujuma”.
Qalibaf ameendelea kubainisha kuwa, Iran ililenga kubadilisha mzunguko uliozeleka wa vita, mazungumzo, na amani kwa kujenga mlingano mpya unaojumuisha vita, mazungumzo, na ngao ya kuhofisha hujuma.
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amehoji kama makubaliano yaliyotiwa saini, ambayo yanajumuisha ahadi za Marekani, yanaweza kuizuia Marekani kuishambulia tena Iran, na akasema: "Bila shaka yoyote, hapana".
Amesema, uadui wa Marekani dhidi ya Iran chimbuko lake ni kubwa mno; na akabainisha kwamba, tabia ya kibeberu ya Washington ya kutaka kutawala na kulazimisha mambo ndiyo inayochochea matashi yake.
"Bila shaka, kama Kiongozi Shahidi [wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei] alivyosema, 'wamekuja ili kuimeza Iran,' " amekumbusha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu.
Amekumbusha pia Muqawama thabiti ilioonyesha Iran wakati wa vita vya kulazimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein kuwa ni mfano dhahiri unaothibitisha umuhimu wa ngao ya kuhofisha yaani deterrence.
"Ile ndiyo maana ya ngao ya kuhofisha hujuma: Asiwepo yeyote wa kuthubutu kutushambulia. Yeyote anayewaza wazo hili la kijinga anapaswa aiangalie tajiriba ya historia na kuelewa kwamba hawawezi kupambana na Iran," amebainisha Qalibaf…/