Somalia: Imarati inaunga mkono makundi ya wabeba silaha na kuchochea machafuko
Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Ahmed Moallim Fiqi, ameituhumu Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuingilia mambo ya ndani ya Somalia, kuchochea migawanyiko ya kisiasa na kuwaunga mkono viongozi wa upinzani wanaoipinga Serikali ya Shirikisho. Tuhuma hizo zimeibuka wakati kukiwa na maonyo kuhusu uhamasishaji wa makundi yenye silaha unaotishia usalama katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu.
Fiqi amewatuhumu baadhi ya wadau wa kigeni kwa kutoa fedha na silaha kwa makundi ya upinzani kwa lengo la kuidhoofisha serikali ya Rais Hassan Sheikh Mohamud na kuzuia juhudi zake za kuimarisha mamlaka ya Serikali ya Shirikisho.
Amesema baadhi ya viongozi wa upinzani wanahamasisha makundi yenye silaha na kukusanya akiba ya silaha katika mji mkuu, Mogadishu. Ameonya kuwa serikali haitavumilia matumizi ya nguvu kwa ajili ya kutimiza malengo ya kisiasa wala vitendo vinavyoweza kudhoofisha utulivu wa nchi.
Waziri wa Ulinzi wa Somalia amesema kuwa watu wenye silaha waliingia katika makazi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Sharif Sheikh Ahmed, akiwatuhumu kuwa walikusanyika hapo kwa lengo la kufanya vitendo vya uchochezi.
“Nyumba ya Sharif imegeuka kuwa kimbilio la machafuko, na wanamgambo wenye silaha wamekusanywa hapo kwa ajili ya kufanya vitendo vya uchochezi,” alisema Fiqi.
Fiqi amesisitiza kuwa Mogadishu haitaruhusu kuwa kituo cha kukusanyika wanamgambo wenye silaha. Amebainisha kuwa, vyombo vya usalama vina wajibu wa kuwalinda raia na kuzuia harakati zozote zinazotishia usalama wa mji mkuu huo.
Amesema vikosi vya serikali vimewaondoa watu 260 wenye silaha katika eneo moja jijini Mogadishu. Aidha, amewatuhumu baadhi ya viongozi wa upinzani kwa kujaribu kuunda makundi yenye silaha na kuhamisha wapiganaji kutoka katika baadhi ya majimbo wanachama wa Serikali ya Shirikisho na kuwaleta katika mji mkuu Mogadishu.
Mapema mwezi Oktoba, Waziri wa Ulinzi wa Somalia aliwatuhumu baadhi ya viongozi wa upinzani kwa kufanya mikutano mjini Abu Dhabi, katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), na makundi ambayo alisema yana uhusiano na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vya Sudan (RSF).